Mahawanga, Amo wang'ara kura za maoni ubunge viti maalumu Dar
Na MWANDISHI WETU
Mjumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga, ametetea kiti chake baada ya kuibuka mshindi kwa kupata kura 448 katika uchaguzi wa kura za maoni ubunge wa viti maalumu.
Mahawanga alifuatiwa na Amina Said Amo, ambaye ni Mkurugenzi wa Amo Foundation, aliyezoa kura 421.
Akitangaza matokeo hayo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, Idrisa Kitwana Mustafa, amesema jumla ya wajumbe walikuwa ni 768.
Ameeleza, kura halali zilizopigwa ni 766 huku kura mbili tu zikiharibika.
Mustafa amemtangaza Janeth na Amo kuwa washindi katika uchaguzi huo huku, Jane Jery Ntate akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 300.
Wengine ni Dorith Kawa alipata kura 119, Maida Waziri (113), Mos Msindo (59), Zainab Janguo (42), Neema Kyusa(21) na Geogina Lukwambe (17).
Mustafa amewataka wajumbe wa mkutano huo kuendelea kuwa wamoja na kuvunja makundi baada ya uchaguzi huo.
Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameitaka UWT kushikamana kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katibu wa UWT Mkoa wa Dar es salaam, Mgeni Otto, amesema wagombea tisa walishiriki uchaguzi huo.
Amesema uchaguzi umefanyika kwa uhuru na uwazi na kuwataka wagombea kuridhika na matokeo, waendelee kukipigania Chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
