Mbeto: Jussa pilipili asoila inamuwashia nini
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, kujiandaa kisaikolojia kwani chama chake hakitamudu kuhimili mikikimikiki ya CCM Oktoba mwaka huu.
Pia CCM imemtaka makamu huyo Mwenyekiti kuacha ngebe na mshawasha huku akiulizwa pilipili iko shamba, Jussa anawashwa na nini mitaani?
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo na kumtaka Jussa ajiandae kushuhudia matokeo yatokanayo na nguvu ya umma ifikapo oktoba Mwaka huu.
Mbeto alimtaka Jussa kuacha propaganda zilizopitwa na wakati huku akidhani atamudu kuwagawa wana CCM kwa porojo zake, uzushi na ufataani wake, badala yake ametakiwa ajue kuwa muda umekwisha na sasa atashuhudia maamuzi ya haki yakipita.
Alisema utendaji wa SMZ uliotokana na ubora wa Sera, Mipango na mikakati thabit ,imetoa matokeo chanya, yenye tija na ufanisi , na sasa hiyo ndio tiketi itakayomrudisha madarakani Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi .
"Kila mcheza kwao hutunzwa, kwa Maendeleo yalioletwa na Serikali ya Rais Dk Mwinyi ,wananachi wameapa kumrudisha madarakani ima faima . Jussa omba uhai ukishuhudie kimbunga Hidaya ' Alisema Mbeto
Aidha, Katibu huyo Mwenezi, aliutaja ushindi wa CCM hautaki tochi, kwani kila mwananchi ameona kazi iliofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar miaka mitano iliopita.
"Rais Dk Mwinyi amemaliza kazi ya kutumikia wananchi miaka mitano iliopita , , jukumu pekee mbele yake ni kukamilisha kazi ya miaka mitano ijayo. Zanzibar itabadilika na kuwa Dubai , Thailand au Hong Kong ya Afrika Mashariki " Alieleza
Akieleza kuhusu madai ya Jussa aliyedai kuwa Rais Dk Mwinyi ametuma wagombea majimboni, Mbeto aliwataka wana CCM kupuuza porojo hizo za kitoto na kusema kazi ya kupandikiza wagombea ni Jussa na wenzake saba ndani ACT Wazalendo.
Aidha, Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Rais Dk Mwinyi walishatangaza hadharani wakiwa jijini Dodoma hawana mgombea yeyote aliyetumwa na viongozi hao kwenye jimbo lolote nchini.
"Dk Mwinyi hajamtuma mgombea yeyote. Kila mwana CCM aliyekwenda jimboni ameamua kwa utashi wake .Wajumbe ndio wenye maamuzi yupi apitishwe kwa mujibu wa sifa zake "Alieleza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema Rais Dk Mwinyi mapema kabisa baada ya kuingia madarakani, aliikataa Siasa za majibizano na malumbano majukwaani, akachagua kazi ya kutumikia wananchi na kujenga Zanzibar kimaendeleo .
Pia Mwenezi huyo alimtaka Jussa aendelee na kazi ya kuwapa matumaini hewa wafuasi wake lakini ukweli wa mambo utajulikana pale wananchi watakapopitisha maamuzi ya kidemomrasia.
