Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania na Airtel zaingia makubaliano kuboresha kilimo
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya Airtel kupitia idara yake ya Airtel Money Tanzania, imesaini makubaliano ya kuingia katika ushirikiano wa kimkakati na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa lengo la kuboresha sekta ya kilimo kupitia huduma za mawasiliano na huduma fedha kidijitali.
Ushirikiano huo unalenga kuwawezesha wakulima kupata huduma salama na za haraka za malipo, kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kupanua upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu, hususan maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano huo, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba alisema kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), kilimo kinachangia takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.
Alisema bado wakulima wengi wadogo hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha hivyo kupitia ushirikiano huu, Airtel Money itatoa suluhisho la malipo ya kidijitali kwa wakulima na vyama vya ushirika, kuwezesha ununuzi wa pembejeo, upatikanaji wa simu janja za bei nafuu, pamoja na kujenga historia ya matumizi ya kifedha.
Alisema watatoa elimu ya fedha na huduma kwa wateja kupitia mtandao wetu mpana wa mawakala.
"Ushirikiano huo unafikiwa kutokana na mafanikio ya majaribio yaliyofanyika na Airtel kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika vya Masoko ya Mazao (AMCOS), mkoani Morogoro, ambapo Airtel Money lengo lake ni kurahisisha malipo ya pembejeo kidijitali", alisema.
Matokeo ya awali yalionesha mafanikio makubwa kwa kuongeza uwazi, ufanisi, na upatikanaji wa huduma kwa wakulima wadogo, huku yakipunguza changamoto za kifedha zilizokuwa kikwazo kwa maendeleo yao.
Rugamba alisema kupitia ushirikiano huo, wanaweza kupanua huduma hizi na kuwafikia maelfu ya wakulima nchini kote ikiwa ni moja wito wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alioutoa Desemba 2023, akiitaka sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na wakulima wadogo ambao wengi wao hulima chini ya ekari 2.5, na wanahitaji msaada wa kubadilika kibiashara.
