Wafugaji wampongeza Rais Dk. Samia kwa utendaji kazi
Na MWANDISHI WETU
Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea chanjo za ruzuku huku wakisema kuwa hatua hiyo inakwenda kuboresha afya za mifugo yao na kuifanya mifugo kuwa na thamani kubwa zaidi soko la kimataifa.
Hayo yameelezwa na wafugaji katika ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchini ikiwa ni wiki mbili baada ya Uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Mrida Mushota alisema, “Chanjo hii ambayo kabla ya ruzuku ya Rais Samia kwa ng’ombe mmoja alikuwa akichanjwa kwa Shilingi Elfu 17 lakini Serikali imesema tutoe 500 tu hiyo nyingine wataibeba wenyewe, mbuzi wetu watachanjwa kwa shilingi 300 tu na Kuku watachanjwa bure lakini pia hapa limejengwa josho la kisasa lililogharimu Mil.28 kwa kweli tunasema Asante Dk. Samia”.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Wilayani Longido, Joseph Sadera aliishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku kwenye chanjo hizo akibainisha kuwa jambo hilo limewaongezea chachu ya kufuga kisasa na kuboresha maisha yao kupitia masoko ya mifugo na mazao yake watakayopata baada ya kuchanja mifugo yao.
Mwenyekiti wa Viongozi wa Mila wilaya ya Ngorongoro na Makamu Mwenyekiti wa CCWT, Kanda ya Kaskazini alisema Rais Samia ameonesha mapenzi makubwa kwa wafugaji kwa kuwapatia ruzuku ya chanjo, na wao wameipokea kwa mikono miwili.
Alisema wafugaji wanachomuahidi ni kuendelea kushirikiana naye katika kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa na mchango mkubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akielezea namna kampeni hiyo itakavyowasaidia kuongeza thamani ya Nyama wanayosindika kwenye kiwanda chao, Mkurugenzi wa kiwanda cha Union Meat, Mariam Ng’hwani alisema chanjo na utambuzi wa mifugo utasaidia kuongeza imani ya bidhaa hiyo kwenye soko la kimataifa.
“Mimi nilikuwa Jaji nchini Ushelisheli lakini baada ya kuona namna mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya Mifugo aliyoweka Rais Dk. Samia niliamua kurudi nchini na kufanya uwekezaji na kupitia hii kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo yetu tayari thamani ya nyama tunayosindika imeongezeka” alifafanua Mariam
Awali, akizungumza wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Arusha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu amewataka wafugaji wote nchini kutumia fursa hiyo iliyotolewa na Rais Samia kupitia ruzuku ya nusu bei kwa upande wa Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo na chanjo ya bila gharama yoyote kwa upande wa kuku wa kienyeji huku akiwahimiza wataalam wote wa Mifugo kutokukaa ofisini na badala yake waende uwandani kutatua changamoto za wafugaji.
Dk. Kijaji aliendelea kufafanua kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani na kukuza diplomasia ya uchumi, mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kufikia Tani Elfu 14 huku akibainisha kuwa lengo la Serikali ni kufikisha Tani 50,000 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, Dk. Kijaji alifafanua kuwa Serikali imeamua kuendesha kampeni hiyo ili kuiwezesha nchi kuuza mifugo na mazao yake kwenye masoko ya nje ambayo awali yalishindwa kutokana na changamoto ya kutokuwa na ithibati ya usalama wa mifugo na mazao yake ambapo amebainisha kuwa tayari nchi za Misri na Falme za kiarabu zipo tayari kuanza kununua mifugo hai kutokana na jitihada hizo.
Tangu utekelezaji wa kampeni hiyo ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ianze rasmi Julai 2, 2025 mpaka sasa, tayari jumla ya mifugo isiyopungua 326,000 imeshachanjwa na kutambuliwa huku lengo likiwa kuchanja ng’ombe takribani milioni 19, Mbuzi na Kondoo milioni 17 na Kuku milioni 40, huku kampeni hiyo ya chanjo ikilenga kukinga mifugo dhidi ya magonjwa ya mapafu ya ng’ombe, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na kwa Kuku ni mafua, mdondo na ndui.