Balozi Mulamula - Utendaji, umahili, weledi na uzoefu wa Balozi Dk Asha Rose Migiro utamsaidia kuipeleka CCM mbele
Na MWANDISHI WETU
Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amempongeza Dkt. Balozi Asha Rose Migiro kwa kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM.
Balozi Mulamula ameyasema hayo, alipozungumzia uteuzi wa kingozi huyo aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
"Nimepokea kwa furaha kubwa uteuzi wa Mhe. Dkt. Balozi Asha Rose Migiro. Naomba kutoa pongezi zangu za dhati kwa kupitishwa na NEC ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa CCM. Pamoja na kwamba nafasi hiyo ni kubwa naamini kabisa kwamba ataimudu barabara kutokana na uzoefu wake na umahiri wake mkubwa na uchapaji kazi,"alisema.
Ameeleza kuwa, aliwahi kupata bahati ya kufanya naye kazi kwa karibu akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na katika nyadhifa mbalimbali.
Amesema anamuaminia sana katika utendaji wake mahiri, uwezo wake na weledi mkubwa kushika nafasi hiyo kubwa ya uongozi wa Chama.
"Namtakia kila la kheri na mafanikio mema katika kulipeleka mbele gurudumu la Chama chetu. Ametoka Balozi anaingia Balozi. amesema.
