CCM IRAMBA WAPONGEZA WATUMISHI WA SHULE YA MSINGI KIOMBOI HOSPITALI UTEKELEZAJI ILANI YA CHAMA


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Iramba, mkoani Singida, Ephraim Kolimba, akizungumza na watumishi na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiomboi Hospitali, wakati wa Mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo, wilayani humo. (Picha na Hemedi Munga).



Na HEMEDI MUNGA 


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Iramba, mkoani Singida, Ephraim Kolimba, amewapongeza watumishi wa Shule ya Msingi Kiomboi Hospitali kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama hicho ya mwaka 2020 hadi 2025.


Kolimba ametoa pongezi hizo wakati wa Mahafali ya wahitimu wa darasa la saba wa shule hiyo iliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo mjini Kiomboi.


Kolimba amewataka Wazazi na Walezi  kuhakikisha wanafunzi hao wanapata chakula pindi wawapo shuleni kwa sababu ni haki yao.


"Kwa kweli katika wilaya yetu haikubaliki  kabisa watoto kukaa bila kula, hivyo sipo  tayari kuulea huo uzembe, niwaombe wazazi wenzangu kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni," amesema.


Pia, Kolimba amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewajengea shule mpya inayoitwa Iramba Sekondari, hivyo wanafunzi hawa ndiyo wakasome katika shule hiyo.


"Kipindi hichi cha Rais wetu ambaye anayetekeleza kila kitu, hatutaki kuona wanafunzi hawapati chakula kipindi wawapo shuleni, ni lazima watoto wapate chakula," amesema.


Katika hatua nyingine, Kolimba amesema Rais alitoa fedha ambazo zimejenga mabweni na vyumba vya madarasa vinne, ambapo watoto wakike watasoma kidato cha tano Shule ya Sekondari Lulumba hivi karibuni.


"Ndugu zangu hakika tunaipongeza sana serikali kwa sababu mbali na shule,  Rais Dk. Samia alitoa zaidi ya sh milioni 250 kukamilisha Zahanati ya Kinambeu, tumependelewa mnno," amesema.


Pia,  ameweka wazi kuwa Chuo cha VETA ujenzi wake unaendelea  kwa kasi kubwa, hivyo hakuna mtoto ataachwa bila ya kupata elimu.


Hata hivyo, Kolimba amekemea tabia inayodaiwa kuzuka ya baadhi ya wahitimu kwenda kufanya kazi za ndani katika majiji ya Dar es salaam na Mwanza, hivyo watakaobainika kufanya hivyo basi watambue kuwa wazazi wao wataishia  jela.


" Urithi wenu watoto wangu ni shule, na serikali imekwishajenga sio tu hapa hata katika mikoa mingine nchini," amesema.


Kwa upande wa Ofisa Elimu Kata ya Old kiomboi,  Daud Mjungu amemuhakikishia Katibu huyo kuwa shule hiyo imeendelea kutekeleza Ilani ya Chama hicho kwa kuhakikisha wanafunzi kwa miaka minne mfululizo wanafaulu kwa zaidi ya asilimia 90.


Hata hivyo, amewaomba Wazazi kuhakikisha wanafunzi hao ifikapo Januari mwakani wanakwenda shule kwa sababu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alikwisha leta fedha ambazo zinajenga shule mpya jirani yao.


"Hakika tunapata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini na Chama kuhakikisha lengo  liliyopo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 ," amesema.


Aidha, amewaomba Wazazi na Walezi kutowakwamisha  wanafunzi hao kwa sababu fursa ya kusoma ipo ambapo serikali imeisogeza huduma hiyo karibu yao na inapatikana bure.


" Ndugu zangu wazazi niwaombe tuwapokee wanafunzi hawa na kuwalea mkifahamu kuwa bado wanasafari ya kuingia kidato cha kwanza Januari 2024," amesisitiza.


Akizungumza na wahitimu hao, mmoja wa Wazazi wa wanafunzi  hao,  Immael Mpondo amewataka kuhakikisha wanakwenda Sekondari  kusoma kwa bidii kwa lengo la kukidhi soko la ajira.


Aidha, amewafahamisha  kuwa siku hizi shule za sekondari  zipo nyingi ikiwemo VETA  ambazo zinawahitaji wanafunzi hao kusoma  hapo, hivyo wakasome kwa bidii na kuepuka vishawishi vinavyodaiwa kuwakatisha tamaa kabla ya kutimiza malengo yao.


"Wazazi wenzagu watoto wasiache shule kwa kisingizio chochote, tuhakikishe watoto wakasome sekondari kwa kuwa Rais Dk. Samia amehakikisha shule zinapatikana kila eneo," amesisitiza.


Pia,  amewataka kusoma kwa lengo la kujiandaa  kupata kazi mbalimbali za ualimu, uhandisi, uwanasheria ikiwemo kuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ambacho hakitatoka madarakani.


Naye Mwanafunzi wa shule ya Hospitali Kiomboi darasa la sita kwa niaba ya wenzake,  Sakina Salumu amewaasa wahitimu hao, kutopuzia yale yote waliyojifunza kutoka kwa walimu wao huku wakimtanguliza Mungu katika maisha yao.


Amewataka kuendelea kuwa na nidhamu ikiwemo kutojihusisha na uvutaji wa bangi, kunywa pombe na kutoiendea zinaa.


Hata hivyo,  amewasisitiza kuhakikisha wanafanya kazi za mikono kwa tumia nyenzo za jembe, nyundo, panga, shoka kwa lengo la kuhakikisha wanafaidi matunda yapatikanayo katika kazi za halali.