WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa madhehebu ya mbalimbali ya dini nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya .
"Tushirikiane kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya ambayo yameathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa."
Majaliwa amesema hayo, alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid lililofanyika Kitaifa jijini Dodoma katika kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete.
“Matumizi ya dawa za kulevya yana madhara mengi kwa Taifa yakiwemo ya kiuchumi, kiafya na kimazingira pamoja na kuathiri uwezo wa mtu kufikiri”
Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini waendelee kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii na wawahamasishe waumini kushiriki katika shughuli zitakazowaongezea kipato.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waendelee kudumisha amani nchini kwa kuwa amani ni jambo la msingi katika maendeleo ya Taifa. "Tuendelee kuishi kwa amani na upendo pamoja na kuliombea dua Taifa na viongozi wakuu. "
Wakati huo huo, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, hivyo waendelee kuiamini Serikali yao.
Awali, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuhu Jabir Mruma amesema kuwa Baraza hizo linaridhishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia za kuwaletea watanzania maendeleo katika Sekta za Uchumi, Siasa, Kijamii pamoja na kuboresha mfumo wa demokrasia nchini.
Aidha, Alhaj Mruma ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iongeze wigo wa kutoa elimu ya uraia kwa kushirikiana na viongozi wa dini ili kuwawezesha wananchi kupata uelewa na washiriki katika chaguzi zijazo ukiwemo wa Serikali za Mitaa inayotarajiwa kufanyika 2024.