Na. WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Oktoba 23, 2023 amezindua Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya (MAB) kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ambayo inawajumbe Saba.
Waziri Ummy wakati akizindua bodi hiyo mpya amewataka wajumbe hao kuimarisha usimamizi wa TMDA katika upande wa dawa, vifaa na vifaa tiba ili kusiwepo na upotevu wa aina yoyote wa vifaa tiba hivyo.
“Kazi kubwa mnayotakiwa kufanya ni ufuatiliaji wa mara kwa mara wa bidhaa duni na bandia zinazoingia kwenye soko ili zisiwafikie wananchi wakazitumia”. Amesema Waziri Ummy
Lakini pia wakati akifungua bodi hiyo Waziri Ummy amewataka wajumbe hao kuharakisha utoaji wa vibali na leseni mbalimbali ili kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wa dawa, Vifaa na Vifaa Tiba.
“Kwakweli niwapongeze kwa hili bodi iliyomaliza muda wake, sikusikia malalamiko ya mtu kucheleweshewa leseni au kibali cha kufanya biashara hivyo bodi hii mpya mkaliendeleze hili”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amepongeza bodi iliyopita kwa kufanya kazi zake kwa weledi ambalo TMDA imepiga hatua kubwa kwenye masuala mbalimbali ndani na nje ya chi na mafanikio ambayo Wizara pia inajivunia kuyafikia na kuitaka bodi mpya kuendeleza mazuri hayo.
“Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kwa bodi iliyopita ni pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi ikiwemo mifumo ya TEHAMA kwenye kutoa vibali vya uingizaji bidhaa nchini ambapo sasa vibali vinatolewa ndani ya masaa 24”. Amesema Waziri Ummy
Bodi hiyo iliyoundwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ina wajumbe Saba ambayo inaongozwa na Mwenyekiti aliyeongezewa muda kwa kipindi kingine Bw. Erick Shitindi, Prof. Appolinary Kamuhabwa (Mjumbe) ambae ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Pia, Bi. Mariam Mwanilwa (Mkurugenzi wa Mishahara na Maslahi ya Watumishi wa Umma-Ofisi ya Rais Utumishi), CPA Chiku Thabit Yusuf (Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu Shirika la Hifadhi ya Jami (NSSF), Wakili Patricia Maganga (Mwanasheria Mbobezi).
Vile vile yupo Bw. Daudi Msasi (Mfamasia Mkuu wa Serikali) na Bw. Adam M. Fimbo ambae ni Katibu lakini pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TMDA.