WANAFUNZI ZAIDI YA MILIONI MOJA KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA NNE





Na Mwandishi Wetu

Wanafunzi 1,692,802 wamesajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne unaoanza Oktoba 25 hadi 26 na wanafunzi 759,573 wa kidato cha pili wakitarajiwa kufanya upimaji huo Oktoba 30,  hadi Novemba 09, mwaka huu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dk.Said Ali Mohamed, amesema shule  za msingi 19,284 zinatarajiwa kufanya mtihani huo kuanzia Oktoba 25 na 26.

Dk.Mohamed amesema kwa upande wa upimaji wa kitaifa kwa kidato cha pili utafanyika kwa shule za sekondari 5,546 Tanzania Bara.

"Jumla ya wanafunzi 1,692 wamesajiliwa  kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, mwaka huu, kati yao wavulana ni 828,591 sawa na asilimia 48.95 na wasichana  ni 864,211 sawa na asilimia 51.05,"amesema.

Amesema kati ya wanafunzi 1,605,379 sawa na asilimia 94.84 watafanya upimaji huo  kwa lugha ya Kiswahili  na wanafunzi 87,423 sawa na asilimia 5.16 watafanya kwa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia kujifunza.

Dk. Mohamed amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu wapo 6,402 kati yao 1,074 ni wenye uoni hafifu, 93 ni wasioona, 1,240 wenye ulemavu wa kusikia, 2,209 mtindio wa ajili  na 1,786 wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Aidha amesema upimaji huo kwa darasa la nne ni  muhimu kwani unawezesha kujua kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi za juu za kusoma, kuandika na kuhesabuKwa upande wa upimaji kwa wanafunzi wa kidato cha pili.

Dk.Mohamed amesema kati ya wanafunzi 759,573  waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili mwaka huu, wavulana ni 353,807 sawa na asilimia 46.58 na wasichana ni 405,766 sawa na asilimia 53,42.

Amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu  ni 1,382 kati yao 683 ni wenye uoni hafifu, 82 ni wasioona, 290 ulemavu wa kusikia  na 309 ulemavu wa viungo vya mwili  na 18 ulemavu wa akili.

Dk. Mohamed amesema maandalizi ya upimaji  kwa wanafunzi hayo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa Kwa karatasi za upimaji na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji katika halmashauri zote nchini.

Amesema umuhimu wa upimaji kidato cha pili, hupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka miwili ya masomo yao ya sekondari, upimaji wa kidato cha nne.

Dk.Mohamed ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa kwani vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza mtihani la Tanzania.

Vilevile amewataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

"Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake", amesema.

Dk. Mohamed amesema wasimamizi wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanafanya upimaji wao ipasavyo, wapate haki yao msingi ambazo ni kupata mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.

Amesema baraza la mitihani halitarajii kuona mwanafunzi yoyote kujiusisha na vitendo vya udanganyifu na kutoa tahadhari kwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

"Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka miwili ya elimu ya sekondari na miaka minne ya elimu ya msingi", amesema.

Aidha Dk. Mohamed amewataka wamiliki wa shule kutambua shule zao ni vituo maalumu vya mtihani na hivyo hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huo.

"Baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo linajiridhisha pasipo shaka uwepo wake unahatarisha usalama wa upimaji wa kitaifa ", amesema.