MSIGWA AZINDUA TAMASHA LA 42 LA SANAA BAGAMOYO

 




Na Mwandishi Wetu


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amefungua rasmi Tamasha la 42 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lililohudhuriwa na wananchi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi  akieleza kuwa Utamaduni na Sanaa ni Sekta zenye  umuhimu mkubwa katika kuleta maendeleo na kukuza ajira hapa nchini.


Katibu Mkuu Bw. Msigwa amesema hayo usiku wa Oktoba 26, 2023 wakati akifungua rasmi tamasha hilo linaloendelea katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).


"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwamba eneo la Sanaa katika nchi yetu ni la kimkakati, ni lazima tulitumie kimkakati. Naomba sana vijana wenye vipaji wasizuiliwe kufanya Sanaa, huku nako kuna ajira" amesisitiza Katibu Mkuu Bw. Msigwa.


Hafla ya ufunguzi wa Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 26 - 28, 2023 katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo Bw. George Yambesi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma, viongozi na wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo.


 Baadhi ya Wasanii na vikundi vilivyofungua tamasha hilo ni Wamwiduka Band, Worrious from the East,  msanii Vitalis Maembe na wengine  wengi.