TTCL YANOGESHA 'TWENZETU KILELENI2023'





Na Andrew Chale, Kilimanjaro.


SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetoa huduma ya bure ya intaneti kwa washiriki watakaopanda mlima Kilimanjaro katika kipindi cha kampeni ya twenzetu Kileleni2023 ambao ni msimu wa tatu.


Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari Mjini Moshi, Kilimanjaro, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, John Yahaya Amesema TTCL wanaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya nchi yetu, kukuza sekta ya utalii sambamba na kuimarisha mawasiliano nchini.


"Washiriki wote watakaopanda mlima Kilimanjaro, katika kipindi hiki cha kampeni ya twenzetu kileleni, watapata fursa hiyo ya intaneti bure wafikapo kila kituo katika mlima huo, ili kutambua umuhimu wa maadhimisho haya ya miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu", amesema. 


Amesema uwepo wa huduma hiyo ya intaneti, itakuwa ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi ya mlima wetu, ndani na nje ya nchi yetu, lakini itahamasisha Watanzania kujenga mazoea ya kutembelea vivutio vya mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya utalii.


Ambapo washiriki zaidi ya 200 watakaopanda mlima huo kwa ushirikiano wa TANAPA na Kampuni ya ZARA tours ambao wanapanda Desemba 5, asubuhi.


Aidha, Amesema kuwa, Shirika hilo limeendelea kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha mawasiliano kwa kuhakikisha kunakuwepo na miundombinu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa katika kutoa huduma ndani na nje.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika ka Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jenerali Mstaafu, George Waitara amewataka Watanzania kujivunia mlima huo kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo  hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika.


Ambapo Amebainisha kuwa, kusherekea uhuru zilianza mwaka 2008 na sasa ni miaka 15 imepita, huku kila mwaka kukiwa na mwitikio mkubwa.


Aidha,Waitara amesema Wasiachie wageni wa nje kuja kuutangaza mlima hivyo kuwataka Watanzania wenyewe kuutangaza mlima huo.


Kwa upande wake Ibrahim Jama, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Makampuni ya Zara tours, amesema zaidi ya watu 200 wanapanda mlima huo kupitia ZARA kutoka katika mashirika na taasisi mbalimbali.


"Tutakuwa na Mabalozi 17, pia mashirika mbalimbali yamehamasika na wanashiriki msimu huu wa tatu wa Twenzetu Kileleni2023", amesema Ibrahim.