WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema idadi ya watu waliokufa kutokana na maporomoko ya udongo wilayani Hanang, mkoani Manyara imefikia 63 na majeruhi 116.
“Kati ya waliofariki wanaume ni 23 na wanawake ni 40. Miongoni mwao, watu wazima ni 40 na watoto ni 23. Kwa watu wazima, wanaume ni 14 na wanawake ni 26; kwa watoto, wa kiume ni tisa na wa kike ni 14,” amesema.
“Majeruhi ni 116 ambapo wanaume ni 56 na wanawake ni 60; miongoni mwao watu wazima ni 60 na watoto ni 56. Kati ya watu wazima 60, wanaume ni 29 na wanawake ni 31 wakati watoto waliojeruhiwa, wa kiume ni 27 na wa kike ni 29,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo kwa Taifa leo (Jumatatu, Desemba 4, 2023) kabla ya kuongoza mamia ya wananchi kutoa heshima za mwisho kwenye ibada ya kuwaaga marehemu hao katika uwanja wa shule ya msingi Katesh ‘A’ wilayani humo.
Ibada ya kuwaaga marehemu iliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Manyara, Sheikh Mohammed Kadidi pamoja na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Baba Askofu Anthony Gaspar Lagwen ambaye alisema Kanisa hilo litachangia sh. milioni tano kwenye mfuko wa maafa.
Akizungumza na waombolezaji hao, Waziri Mkuu aliwafikishia salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwajulisha kuwa ametoa maelekezo kwamba Serikali isimamie kwa namna yoyote ile masuala ya wafiwa na majeruhi na kuhakikisha kuwa wote walionusurika wanahudumiwa.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza kwamba huduma za miili itafanywa na Serikali kwa kutoa majeneza na usafiri hadi makwao ili kila mmoja akazikwe kwa taratibu za kimila na kifamilia. Kwa majeruhi wote, matibabu yatolewe bure hadi wapone na kurejea kwenye hali zao,” amesema.
“Mbali na majeruhi, kuna watu nyumba zao zimesombwa; hawa ameelekeza wawekwe kwenye kambi maalum, ambazo nimeambiwa ni shule tatu na wapewe chakula, maji na huduma za matibabu endapo italazimu.”
Waziri Mkuu amesema leo imeagwa miili ya watu 52 ambayo tayari ilikuwa imeshaandaliwa na kesho asubuhi (Desemba 5, 2023) litafanyika zoezi la kuaga miili iliyobakia. Alisema ili kuwe na uratibu mzuri, taarifa za kila siku kuhusu tukio hilo, zitatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga na kwamba rambirambi zote zielekezwe kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Kabla ya kushiriki kuaga marehemu hao, Waziri Mkuu alikwenda kukagua sehemu ambayo imeathirika zaidi ambako nyumba zote za kijiji cha Gendabi zilisombwa na maji na kubakizwa Kanisa tu. Pia alikagua kwa helikopta na kujionea athari za mafuriko hayo kwenye mji mdogo wa Katesh. Maeneo mengine yaliyoathirika ni Jorodon na Ganana.
Amezishukuru Kamati za Maafa za Wilaya na Mkoa ambazo zilianza kuchukua hatua za uokoaji tangu jana, lakini pia mawaziri na watendaji wao ambao walikuja kutoa msaada kwa kuungana na viongozi wa mkoa wa Manyara.
Mapema, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Annamringi Macha aliwasilisha salamu za pole na kusema kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa maafa hayo.
Alisema wamekabidhi mchele (magunia manne) maharage (magunia 9), unga wa sembe (viroba 100 vya kg.25), katoni za maji 150 na sabuni ambavyo vyote alisema vina thamani ya sh. milioni 10.