DAR ES SALAAM, SEGERIA
Wanawake wa Jimbo la Segerea, Ilala, Jijini Dar es Salaam, wamechangishana sh. milioni 4.5 kwajili ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuchukua fomu ya kugomnbea urais muhula wa pili mwaka 2025.
Wanawake hao wamechanga fedha hizo leo katika Kongamano la Wanawake Jimbo la Segerea, kumpongeza Rais Dk. Samia, kutimiza miaka mitatu ya uongozi wake ambapo pia walifanya maandamano ya kumpongeza Rais Dk. Samia.
Kongamano hilo liliandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Segrea, Bonnah Kamoli, ambaye amesema katika Uchaguzi MKuu wa Mwaka 2025, wanawake Segerea wana jambo lao kuhakikisha Rais Dk. Samia anashinda kwa kishindo.
Amesema, katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya Rais Dk. Samia madarakani, Jimbo la Segerea limepiga hatua kubwa katika sekta zote muhimu, hususan, elimu, afya, miundombinu, maji na kusisitiza wanawake jimboni humo kupatiwa mikopo kwani vikundi vingi ambavyo vilisajiliwa kupata mikopo ya asilimia 10 iliyokuwa ikitolewa na halmashauri ambayo ilisitishwa havikupata mikopo hiyo.
Bonnah amesema kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia katika jimbo hilo, wanawake wanapaswa kumuunga mkono kwa kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba kuelekea uchaguzi wa 2025 wanamsaidia kuchukua fomu kwa kumchangia kwa hiyari kiasi chochote.
Katika hotuba hiyo, Bonnah aliwataka wanawake waliohudhuria kongamano hilo kwa hiyari yao kumchangia Rais Dk. Samia, fedha za kuchukulia fomu ambapo kilipatikana kiasi cha sh.milioni 4.5 zilizo kabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alikuwa ni mgeni rasmi.
Akipokea fedha hizo, Mpogolo, amewashukuru wanawake wa Jimbo la Segerea na Mbunge Bonnah , kwa kumuunga mkono Rais Dk. Samia na kuwataka kushikamana kuhakikisha Rais Dk. Samia anaongoza miaka mitano mingine.