Na MWANDISHI WETU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka vijana kuwa wazalendo kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kudumisha Demokrasia na kushiriki katika chaguzi kwa kupiga kura katika chaguzi za mitaa, vijiji na vitongoji.
Amesema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano mzuri wa Demokrasia hata kukubali uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 nchini na kukubali kung'atuka katika madaraka jambo ambalo siyo lakawaida kwa viongozi waliopigania uhuru wa nchi zao.
Mpogolo ameyasema hayo alipozungumza kuhusu maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Amesma ili kumuenzi Nyerere na kuendelea kumkumbuka ni vema vijana wa Tanzania kudumisha amani, umoja, mshikamano na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Ameeleza miaka 25 ya kifo cha Mwalimu vijana wanatakiwa kujifunza maisha ya Mwalimu Nyerere aliyependa utu, kujifunza na kutosheka katika madaraka hali iliyomjengea heshima ya kisiasa nchini, barani Afrika na dunianiani kwa ujumla.