Na MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Geita Mjini Costantine Kanyasu ameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuzitumia benki ndogo za ndani kufanya malipo wakati wafanyabiashara wanapowauzia dhahabu kurahisisha biashara.
Kanyasu ameyasema hayo, wakati wa kufunga maonesho ya saba ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini Mkoa wa Geita ambapo alitoa ombi hilo kwa niaba ya wafanyabiashara wa dhahabu.
Amesema kuwa kutokana na uwepo wa soko la dhahabu Geita, wafanyabiashara wa dhahabu wapo tayari kuiuzia BoT dhahabu lakini wameiomba itoe idhini kwa benki za hapa nchini kuchakata malipo yao.
“Kutokana na uwepo wa soko hili sasa hivi tumeanza kununua dhahabu kwa ajili ya Benki Kuu, ombi moja kutoka kwa wafanyabishara wa dhahabu, wapo tayari kuwauzia Benki Kuu lakini wanaomba benki kuu itoe fedha zake kwenye benki ambazo ni za kawaida kuliko kusubiri benki kuu ndio waanze kuchakata malipo,” alisema Kanyasu.