MUHIMBILI MLOGANZILA YAPANDIKIZA NYONGA NA MAGOTI KWA WAGONJWA 13, MATUNDU MADOGO YATUMIKA

Na MWANDISHI WETU

Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari Bingwa Mbobezi wa Upandikizaji Nyonga na Magoti kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth ya nchini Uingereza Prof. Mamoun AbdelGadir imefanya upasuaji wa kupandikiza nyonga na magoti kwa wagonjwa 13 ambapo baadhi yao wamefanyiwa huduma hiyo kwa kutumia njia ya kisasa ya matundu madogo.

Upandikizaji huo umefanyika kupitia kambi maalum iliyofanyika hospitalini hapo kuanzia Oktoba 21 hadi 25,2024 ambapo pamoja na upandikizaji huo wagonjwa wenye changamoto za nyonga na magoti wamefanyiwa uchunguzi, kupewa ushauri, matibabu na wengine wamefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa magoti na nyonga kulingana na ukubwa wa matatizo waliyonayo.

Katika kambi hii wataalam wa ndani walipata fursa ya kujengewa uwezo wa kutoa huduma ya upandikizaji wa nyonga na magoti kwa kutumia njia ya matundu madogo ambayo ni teknolojia mpya kwa hospitali za hapa nchini.

Kutolewa kwa huduma hizi za ubingwa bobezi hapa nchini ni mwendelezo wa Serikali wa kuboresha huduma za afya nchini na kuwaondolea usumbufu Watanzania kutafuta matibabu haya nje ya nchi ikiwemo gharama na muda wa kutafuta matibabu ya aina hii.

Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeshafanya upandikizaji wa nyonga na magoti kwa wagonjwa 205 tangu huduma hizo zilipoanza kutolewa  hospitalini hapa mwaka 2022.