MULAMULA -KUJIANDIKISHA NI HAKI YENU MPATE FURSA YA KUPIGA KURA KUWACHAGUA VIONGOZI BORA MNAOWATAKA

Na MWANDISHI WETU

BALOZI Liberata Mulamula, amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kujiandikisha katika daftari la Mkaazi  jambo linaloendelea kwasasa nchini kote kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa.

Balozi Mulamula ametoa ujumbe huo jijini Dar es Salaam, alipofika kujiandikisha katika Daftari la Mkaazi, Kata ya Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni.

Amesisitiza kuwa, ni muhimu kila Mtanzania akajitokeza kuhakikisha anajiandikisha katika Daftari la Mkaazi  la mpiga kura, kwani ndiyo haki yake ya msingi ya kikatiba inayomwezesha kupata fursa ya kupiga kura.

"Tunaendelea kuwahamasisha wananchi kila sehemu tunapokuwa, kuhakikisha wanatumia haki na fursa yao hiyo ya msingi, tunawaomba viongozi wa dini watusaidie kuwahamasisha wananchi wajiandikishe kupata fursa ya kuwachagua viongozi wanao wataka wakati ukifika," amehimiza.

Pia, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Rais Dk.samia Suluhu Hassan katika kazi nzuri inavyoendelea kuzifanya na kumwombea afya njema kiongozi wa nchi, aendelee kutekeleza majukumu yake.