Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Tangu kuanzisha kwake mwaka 1974.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam jana katika Pastorate ya Magomeni na Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Pwani, Philip Magwano, ambapo alisema maadhimisho yanatarajiwa kufanyika Oktoba 27 kanisani hapo Magomeni.
"Mgeni rasmi katika jubilee yetu hii ya miaka 50, anatarajiwa kuwa Rais wetu, Dk.Samia Suluhu Hassan, ambapo atazungumza na waumini wa kanisa hili na Watanzania kwa ujumla.
"Tutafurahi kwa hatua hii na tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kukubali kuwa mgeni rasmi, kukubali mwaliko wetu, kwani ni kiongozi bora anayependa watu wa dini zote, kabila zote na makundi mbalimbali ya kijamii anayesisitiza amani na upendo, tuna mpenda, tunaendelea kumwombea heri," amesema.
Askofu Magwano, amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamechangia kanisa hilo, hali iliyowezesha ukarabati huo unaoendelea wa kuboresha jengo la kanisa hilo.