BASHUNGWA AWAJULIA HALI MAJERUHI 16 AJALI BIHARAMULO, ABIRIA 11 WAFARIKI DUNIA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amefika eneo ilipotokea ajali ya basi la abiria lenye namba za usajili T857 DHW, katika eneo la Kabukome, Kata ya Nyarubango wilayani Biharamulo mkoani Kagera na kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupewa matibabu katika hospitali teule ya biharamulo, tarehe 21 Disemba 2024.

Basi hilo liliokuwa linafanya safari kutoka Kigoma kwenda Bukoba, liliposimama kushusha abiria aliyepitilizwa katika kituo, lilishindwa kuondoka na kuanza kurudi nyuma kisha kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo imesababisha vifo vya abiria 11 na majeruhi 16 ambapo majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali teule ya Biharamulo mkoani Kagera.

Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi, Bashungwa ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.

“Nitumie nafasi hii kuombea raho za marehemu ambao tumewapoteza katika ajali ambayo imetokea hapa Biharamulo, tumepoteza ndugu zetu 11, wametangulia mbele za haki”, amesema Bashungwa

Aidha, Bashungwa amesema Wizara imeanza kufanyia kazi maelekezo ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ya kufanya marekebisho ya kuwa na mfumo wa leseni za udereva,  kuwapunguzia alama madereva wanafanya makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani ambazo zitapelekea kuwafungia leseni.

Kwa Upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali teule ya Biharamulo, Gresmus Sebuyoya, amesema majeruhi 26 wameruhusiwa na wengine 16 wanaendelea na matibabu na ungalizi wa karibu.

“tumebaki na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, wanaume tunao sita, vifo tulikuwa navyo kumi na moja, wanawake watano, wanaume wanne na watoto wawili” ameeleza Daktali Gresmus.