MBUNGE KIGAHE AFANIKISHA MIRADI YA MAJI MUFINDI KASKAZINI



Na MWANDISHI WETU

Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe ambaye ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, ameendelea kutatua kero ya wananchi kwa kutekeleza miradi ya maji jimboni humo.

Kigahe ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi jimboni humo, baada ya kushuhuda utekelezaji wa Mradi wa Kisima kirefu cha maji safi na salama katika Kijiji cha Ihimbo Kata ya Mapanda Jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa.

"Mradi utakapokakamilika utawasaidia sana wananchi hao kupunguza adha ya kufuata maji bondeni ambayo siyo safi na salama kiafya. Hivyo, kupitia mradi huu wananchi watanufaika moja kwa moja katikà matumizi ya kawaida na fursa zingine kama Kilimo," alisema.

Alieleza kuwa, katika historia ya Jimbo hilo, Kijiji hicho hakijawahi kuwa na Mradi wowote wa maji safi na salama, hivyo ndiyo maana akafanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Mbunge Kigahe alimshukuru Rais Dak. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha, huku akiwapongeza viongozi na watumushi wote wa serikali na Wananchi jimboni humo kwa kufanikisha kukamilika mradi huo.