MSIGWA ASISITIZA WASAFIRISHAJI KUZINGATIA SHERIA BARABARANI KUEPUKA AJALI

 


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali, amewataka wasafirishaji hususan wale wa mabasi yaendayo mikoani kuzingatia kanuni na sheria za usafirishaji kuepuka ajali katika kipindi hiki cha kuelekea siku kuu za mwisho wa mwaka.

Pia, wasafirishaji kuepuka upandishaji wa nauli katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ambacho watu wengi husafiri, kwani tayari mifumo ya ukataji tiketi inaendelea kuandaliwa kuepuka upandishaji wa nauli kiholela ambazo hufanywa na wasafirishaji wasio waaminifu.

Msigwa ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam, alipotembelea kituo cha ufuatiliaji wa mienendo ya mabasi ya abiria yaendayo mikoani (VTS), kilichopo Mikocheni.

"Nimefurahi kutembelea kituo hiki cha LATRA cha kufuatilia mfumo wa mwenendo wa magari barabarani (VTS) kilichopo hapa mikocheni kushuhudia uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na serikali kuboresha usafirishaji," amesema.