RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, walioko vituo mbalimbali nchini viwasaidie katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismas Mwaka Mpya.
Baadhi ya zawadi zilizotolewa ni sukari, mafuta, unga, mchele, vinywaji na vitoweo na mahitaji mbalimbali ya watoto.
Akikabidhi zawadi hizo katika Kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Msimbazi Center, kilichopo chini ya Kanisa la Roman Catholic, Msaidizi wa Rais Dk.Samia katika masuala ya siasa, Benedict Kikove, amesema ni utamaduni wa kiongozi huyo wa nchi kufanya hivyo kila ifikapo kipindi kama hicho kufurahi na makundi hayo.
"Imempendeza Rais Dk.Samia kutoa zawadi hizi kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wafurahie siku kuu hizi za Christmas na Mwaka Mpya.
"Kama ilivyo Utamaduni wa Rais Dk.Samia kufanya hivi vipindi mbalimbali vya siku kuu, hivyo na leo ameona ufurahie siku kuu ya Noel na wajukuu zake hawa, kupitia zawadi hizi mbalimbali ikiwemo kitoweo," amesema.
Ameeleza kuwa, Rais Dk.Samia ametoa zawadi hizo ikiwemo sukari, vitoweo na mahitaji mbalimbali katika vituo vyote nchini, kwa lengo la kuendelea kuwahimarisha afya zao kimwili na kiroho wajukuu zake hao.