Airtel Tanzania yatoa Mafunzo ya Ujuzi wa kidijitali kwa walimu kupitia Mpango wa SmartWASOMI
Na MWANDISHI WETU
Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation kwa kushirikiana na UNICEF, Wizara ya Elimu, imeandaa warsha ya mafunzo kwa walimu wa IT chini ya mpango wa Airtel SmartWASOMI.
Mradi huo wa kisasa wa ujifunzaji wa kidijitali unaolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora kupitia teknolojia.
Warsha hiyo imewakutanisha walimu 60 kutoka shule za msingi na sekondari ambazo tayari zimeunganishwa na mpango huo.
Mpango huo ulizinduliwa Mei 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ikiwa ni ushirikiano kati ya Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation, UNICEF na Serikali ya Tanzania.
Zaidi ya shule 400 kote nchini zimeunganishwa na jukwaa hilo, likiwa na huduma ya bure ya mtandao (zero-rated) kwa majukwaa ya mitaala ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Shule Direct, hivyo kuwapa maelfu ya wanafunzi na walimu fursa ya kupata rasilimali za ujifunzaji wa kidijitali bila gharama za data.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisisitiza umuhimu wa walimu katika mafanikio ya mpango huo.
“Walimu ndio msingi wa mfumo wetu wa elimu, lengo la warsha hii ya mafunzo ni kuongeza uwezo wa walimu katika kufundisha kwa njia ya kidijitali na kuboresha matokeo ya elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Tunawekeza kikamilifu katika kuboresha elimu kupitia kuwaandaa walimu kutoa elimu bora inayojumuisha matumizi ya teknolojia,” alifafanua.
Singano aliongeza kuwa Airtel SmartWASOMI imeondoa kikwazo kikubwa cha ujifunzaji wa kidijitali kwa kutoa huduma ya kuingia kwenye maudhui ya elimu bila gharama ya data kupitia mtandao wa Airtel, hivyo kuwapa wanafunzi na walimu njia rahisi na ya uhakika ya kufikia vifaa vya kujifunzia vilivyokubaliwa na serikali.
