Dk.Mafumiko aanika mafanikio ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali
Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imesema katika miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inajivunia uwekezaji mkubwa wa mitambo na vifaa vya kisasa vilivyo boresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara wenye thamani ya sh. bilioni 17.8 ikiongeza mitambo mikubwa 16 na midogo 247.
Pia, alisema katika kipindi hicho wamefanikiwa kuongeza uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kutoka sampuli 155,817 kwa mwaka 2021/22 kufikia 188, 362 kwa mwaka wa fedha 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 21, huku kipindi cha mwaka huu wa fedha kufikia Mei, sampuli 175,561 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 92 ya lengo la kuchunguza sampuli 191,420.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, katika Mikutano na Wahariri na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Fedelice Mafumiko, alisema uwekezaji huo ni sawa na ongezeko la asilimia 23.6 ukilinganisha na uwekezaji wa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/2022 uliokuwa na thamani ya sh. bilioni 13.6.
Dk. Mafumiko alisema uwekezaji huo umewawezesha kuwa ni maabara ya pili kwa ukubwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ikitanguliwa na ile ya Tunisia, huku wakiwa wamepata Ithibati ya umahiri wa uchunguzi kimataifa.
"Utoaji Huduma za Kimaabara katika Viwango vya Kimataifa Katika kipindi cha Serikali ya Rais Dk. Samia, Mamlaka imefanikiwa kuendelea kutoa huduma za Uchunguzi wa Kimaabara na matokeo yake kukubalika katika ngazi na Viwango vya Kitaifa na Kimataifa.
“Kukubalika huko kwa matokeo ya uchunguzi kunatokana na Mamlaka kutekeleza mifumo miwili ya ubora na umahiri ya kimataifa, ambayo ni Ithibati ya Mifumo ya Usimamizi wa Ubora (ISO 9001:2015) ya uendeshaji wa shughuli za Mamlaka uliyohuishwa mara nne mfululizo na mfumo wa Ithibati katika Umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2027),”alisema Dk. Mafumiko.
