Segerea yaitika Bonnah akichukua fomu za uteuzi ubunge
Na MWANDISHI WETU
Wanachama, wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi katika Jimbo la Segerea, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, leo wamejitokeza kumsindikiza Mgombea Ubunge wa jimbo hilo Bonnah Kamoli, kuchukua fomu ya uteuzi katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wilayani humo.
Msafara wa magari, pikipiki na bajaji wa mgombea huyo uliopambwa kwa shamrashamra, ngoma, matarumbeta na nyimbo za kuisifu CCM ulianzia katika eneo la Tabata Shule, saa 6:00 mchana, kupitia Tabata Segerea, kisha kuingia Barabara ya Segerea-Majumba Sita na kuingia Barabara ya Nyerere kisha Mtaa wa Lumumba zilipo ofisi ndogo za INEC.
Bonnah, alipanda gari linalofunguka kwa juu na kujitokeza katika paa la gari hilo huku akipunga mkono na kupeperusha bendera ya CCM katika mitaa msafara huo ulipopita.
Mgombea huyo alikabidhiwa fomu na Msimamizi wa Uchaguzi wa INEC katika majimbo ya Segerea, Kivule, Ukonga na Ilala, Faraja Nakua.
