WCF yatoa mafunzo kwa madaktari Kanda ya Ziwa
Na MWANDISHI WETU
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendesha mafunzo kwa madaktari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Jijini Mwanza, yamelenga kuwaongezea wataalamu hao weledi katika kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi wanaopatwa na changamoto hizo.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisisitiza umuhimu wa madaktari kupata uelewa wa kitaalamu kuhusu masuala ya afya ya wafanyakazi, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha haki za wafanyakazi zinazingatiwa kupitia tathmini sahihi za kitabibu.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa WCF katika kulinda ustawi wa wafanyakazi, aliongeza kuwa mafunzo haya yatawawezesha madaktari kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za utofauti wa maamuzi ya kitabibu, hivyo kulinda nguvu kazi ya taifa”, alisema
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Anselim Peter, alibainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma kwa wakati, kwa ubora na kwa usahihi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF Dk. Abdulsalaam Omary alisema kuwa dhamira ya WCF kuongeza idadi ya madaktari wanaopata mafunzo ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
