SPIKA DKT. TULIA AKABIDHI MISAADA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG, AMPONGEZA RAIS SAMIA

 



Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Desemba 6, 2023 ametembelea eneo  lililoathirika kwa mafuriko na maporokoko ya tope na magogo Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara na kukabidhi misaada mbalimbali  kwa waathirika wa mafuriko hayo.



Misaada iliyokabidhiwa kwa niaba ya Bunge la Tanzania na kupokelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, Jenista Muhagama ni Kilo 3000 za mchele, kilo 3000 za Unga, Maharage kilo 800, mafuta ya kula lita 500, katoni 13 za sabuni na sabuni ya unga viroba 30. 


Wakati huohuo Dkt. Tulia alipata fursa ya kuwatembelea na kuwapa pole waathirika wa mafuriko hayo wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo. Aidha, ameipongeza Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutoa huduma za kibidamu kwa haraka hususan matibabu bure kwa wahanga hao.


Baada ya kupokea misaada hiyo, Mhe. Jenista amempongeza na kumshukuru Dkt. Tulia na kwa namna ambavyo Bunge limeguswa na janga hilo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha misaada yote iliyotolewa inawafikia waathirika wote. 


Vilevile Jenista amempongeza Dkt. Tulia kwa unyenyekevu wake wa kufika na kuwafariji wagonjwa wa janga hilo,  kitendo alichokiita ni  mfano bora na wa kuigwa na Viongozi wengine.