TMA YAKAMILISHA UBORESHAJI WA RADA MBILI ZA HALI YA HEWA

Na MWANDISHI WETU, Dar es salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekabidhiwa rasmi ya rada zake mbili za hali ya hewa zilizopo Mwanza na Dar es salaam zilizokuwa zinafanyiwa uboreshaji na kampuni ya Enterprises Electronic Corporation (EEC) kutoka Alabama, Marekani (USA).

Maboresho hayo  yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia bajeti ya maendeleo yalilenga kuboresha (upgrading) ufanisi wa rada hizo zilizokwisha tumika kwa zaidi ya miaka 10 kwa kutoa vifaa vyenye teknolojia yenye software ya kizamani (edge 5) na kufunga ya kisasa (edge 6), kupata picha nzuri itakayoweza kutafsiriwa kiurahisi.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ofisi za rada ya Dar es Salaam, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa TMA, OFISI YA Zanzibar, Masoud Faki, alisema amefuatilia kwa karibu muonekano wa picha za rada ya Bangulo, Dar es Salaam, ameonesha kuridhishwa kwa maboresho ya vifaa vilivyohuishwa na kufanya rada hizo kuwa na uwezo mzuri wa kuona matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini ikiwemo vimbunga endapo vitajitokeza Baharini ili kuwatahadharisha wakazi wa eneo husika.

" Kwa kweli nimeridhishwa na namna ambavyo hizi 'instruments' (vifaa) zimekuwa 'replaced' na kuona sasa rada zinaweza kufanya kazi kwa kupata 'product' (picha) zenye 'high resolution' (muonekano mzuri) hadi baharini hivyo tunatarajia zitatusaidia katika ku 'predict' (kutabiri) hali mbaya ya hewa ili kuokoa jamii yetu dhidi ya majanga ya hali mbaya ya hewa". Alisisitiza Masoud.