WANAWAKE TUMIENI WINGI WENU KUHAKIKISHA MNASHINDA JAMBO LENU OKTOBA MWAKA HUU

 

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa.

Na HEMEDI MUNGA, Iramba

Wanawake wametakiwa kutumia wingi wao kuhakikisha wanashinda katika jambo lao ifikapo Oktoba mwaka huu.

Wito huo, ameutoa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa wakati wa semina kwa viongozi kuhusu Mafunzo ya Usambazaji na Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kizaga wilayani Iramba, mkoani Singida.

Akizungumza na viongozi hao, Dk. Albina alisema takwimu zinaonesha wilayani hapo, wanawake wanaongoza  kwa sababu wapo 165, 000 na wanaume 163,000.

"Tunakazi wanawake wenzangu, tumesoma, tuna sera ya 50 kwa 50, hivyo tukachukue fomu kwa sababu takwimu zimekwishatuonesha," amesema.

Katika hatua nyingine, ameeleza kiwango cha watu kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea wanaojua kusoma na kuandika kimeongezeka hadi asilimia 83.

Amesema wamepiga hatua kufikia kiwango hicho ukilinganisha na asilimia takribani 44 kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Aidha, ameweka wazi Mkoa wa Singida una asilimia 70 huku kwa wilaya ya Iramba wakiwa asilima 68  ya watu wanaojua kusoma na kuandika kwa lugha yoyote.

Amesema hatua hiyo ni kubwa, hivyo waungane na serikali yao kwa kwenda kuzifanyia kazi takwimu ambazo wamepewa.

Kwa upande wa mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, amesema Rais Dk. Samia anabebwa na takwimu zinazoeleza mambo mbalimbali aliyoyafanya nchini.

Ameeleza kwamba wakati anateuliwa kuiongoza Iramba, alikuta vijiji 54 ndio vyenye umeme huku hivi sasa vijiji vyote 70 vya wilaya hiyo vinaumeme.

Ameongeza vitongoji 189 vinanishati hiyo huku akiweka wazi kuwa wananchi hao wanapata ruzuku toka serikalini pindi wanapolima.

"Furaha ya mara mbili  wanayoionesha wananchi wangu imeletwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan," amesema DC Mwenda.

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), anayewakilisha wanawake wa Mkoa wa Singida, Grace Mkoma, amemshukuru Dk. Albina kwa kuanzia wilaya hiyo kutoa elimu itokanayo na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Aidha, amewataka viongozi hao kwenda kuyafanyia kazi yote waliofundishwa ikiwemo kuifikishia jamii inayowazunguka.

Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), anayewakilisha wanawake wa mkoa wa Singida, Grace Mkoma.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Suleiman Mwenda.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda (kulia).