MKOLWE: UWEKEZAJI WA BANDARI UNA TIJA KWA TAIFA


NA MWANDISHI WETU

Ni ukweli kwamba Tanzania ni miongoni mwa maeneo ya dunia yaliyopendelewa kwa kiasi kikubwa na Mwenyezi Mungu.

Kupendelewa huko kunatokana na kuwa miundombinu mingi ya asili ambayo endapo ikitumika vizuri inaweza kuleta faida na maendeleo kwa faida ya Taifa la Tanzania na wananchi wake.

Hayo ameyasema Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa Vijana  wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, Salum Mkolwe, wakati akizungumza na mwandishi wa habari.

Amesema kwa sasa watanzania wanatakiwa kuacha malumbano katika mambo ambayo yako wazi kuwa uwekezaji wa bandari nchini utakuwa na tija katika nyanja mbalimbali.

Mkolwe amesema kitu kikubwa ambacho Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan,  imekuwa ikijitahidi ni kutafuta ajira kwa wananchi wake hususan vijana kwa kufungua sekta ya biashara na kilimo,  hivyo uwekezaj unaotaka kufanywa na Kampuni ya DP Word ya Dubai katika uendelezaji na uendeshaji wa bandari unaweza kuleta ajira nyingi kwa Vijana.

Amesema wanavyoisoma kampuni ya DP Word inauwezo mkubwa wa kuifanya bandari kuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia wafanyabiashara wengi tena kwa muda mfupi.

" DP World ni Kampuni kubwa inayoweza kuhudumia wateja wengi Bandarini kwa muda mfupi, hivyo watanzania hawana haja ya kuogopa tuunge mkono" amesema Mkolwe.

Amesema duniani hakuna mkataba usio na kikomo na kuvunjwa pale unapokiukwa au unapotakiwa kufanyiwa marekebisho hivyo wasitishwe na wananchi wachache ambao hawana nia njema ya kuhakikisha Tanzania inapiga hatua. 

"Nchi yetu ina wanasheria nguli na wenye weledi katika masuala ya mikataba ya uwekezaji baina ya Serikali na Sekta binasfi kutoka nje ya nchi, hivyo wakati wa kusaini mikataba mahususi na kampuni ya DP World ni dhahiri kila jambo litafanyika kwa mujibu wa sheria na kuweka maangalizo ambayo hayana madhara kwa Taifa" ameongeza Mkolwe.

Pamoja na hayo Uwekezaji huo utaifanya Bandari kuwa lango kuu la uchumi wa mataifa ya DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Uganda na Malawi ambapo uletaji wao mizigo utakuwa na manufaa kwa taifa katika suala zima la kuongeza mapato.

Pia Mkolwe amemuomba Mh. Rais Samia kuendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi katika Sekta mbalimbali,  kuendelea kupata mapato yatokanayo na uwekezaji na hatimaye faida itakayopatikana ichangie katika bajeti kuu ya Serikali na hatimaye kuwa chachu ya maendeleo kwa Taifa.