WAHITIMU TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA

Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dk. Naomi Katunzi.

 Na Mwandishi Wetu

Wahitimu wa Shahada, Stashahada na Astashahada za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), wametakiwa kudumisha, kuthamini utu wa mtanzania kwa kuwa mabalozi wema kimaadili, nidhamu kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa wa Baraza la Usimamizi la TEWW, Dk. Naomi Katunzi, wakati wa Mahafali ya 60 ya taasisi hiyo katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam, jana.

Naomi amesema wajiepushe na vitendo vya rushwa, ubinafsi na ubadhilifu hasa katika utumishi wa umma wawe raia wema na kuigwa katika utendaji kazi zao.

Amesema wahitimu hao wakatumie taaluma waliyoipata kwa kuhakikisha wanakuwa chachu ya maendeleo chanya kwa taifa, pia wajiepushe na kuchukua tahadhari katika maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwakua taifa na familia zao bado zinawahitaji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Profesa Michael Ng'umbi.

Pia Naomi alipomngeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi anazozifanya kuendeleza sekta mbalimbali nchini, ikiwemo sekta ya elimu hususan kutambua vijana walio nje na shule.

"Taasisi hii ninayoishi imepewa dhamana ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu ya watu wazima na zinazotolewa nje ya mfumo rasmi", amesema.

Amesema serikali imeendelea kuboresha miundombinu  kwa kupitia mradi wa Kuimalisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambao umeweza kujenga majengo katika mikoa sita nankufanya ukarabati mkubwa katik majengo ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Naomi amewaasa TEWW kutumia vizuri fedha wanazopewa na serikali kwani watambue kuwa watanzania wana kiu ya kupata elimu, ikiwemo wahitaji wanaotoka katika makundi maalumu, hususan vijana walio nje ya shule ambao wana haki ya kupata elimu pamoja mazingira bora ya kujifunzia na miundombinu ya kisasa.

Wahitimu wakiwa katika maandamano ya Mahafali ya 60 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo TEWW, Profesa Michael Ng'umbi, ameishukuru  serikali kwa kuendelea kuiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake.

"TEWW inaongozwa na Mkakati wa Kitaifa wa Kimasomo na Elimu kwa Umma (NALMERS) na miongozo mbalimbali ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa elimu hasa elimu ya watu wazima na elimu ya nje ya mfumo rasmi", amesema.

Pia Ng'umbi amesema uwepo wa programu za Shahada, Stashahada na Astashahada, umewezesha taasisi hiyo kuwandaa walimu na wasimamizi wa EWW ambao wana ujuzi na utayari wa kwenda kuanzisha au kuendeleza kimasomo.

Amesema TEWW inakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha, hali inayosababisha kushindwa kutekeleza kwa ufanisi baadhi ya majukumu yake, hivyo ameiomba serikali kuendelea kuipa fedha.

Wahitimu wakifuatilia hotuba za viongozi mbalimbali katika mahafali hayo.