WAZIRI MKUU AWAHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO



 
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini washiriki katika michezo kwa kuwa michezo ni ajira, uchumi na huimarisha afya.

“Tunapa faida nyingi kwa kufanya michezo, tushiriki katika michezo pamoja na kukimbia riadha kwa kuongeza vipaji tulivyonavyo kwani tukishindana tunapata na zawadi. Michezo ni uchumi. “ 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 9, 2023) baada ya kuzindua Ruangwa Marathon katika kiwanja cha Kilimahewa, wilayani Ruangwa Lindi.

Aidha, Waziri Mkuu amesema amemshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika sekta ya afya nchini ikiwemo na wilaya ya Ruangwa.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya kutolea huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afyfa na hospitali ya wilaya ambayo inavifaa tiba vya kisasa.

Mbio hizo za hisani ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza wilayani Ruangwa zimehudhuriwa na wanariadha mbalimbali wanaoliwakilisha Taifa katika mashindano ya mbio za kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel amesema mbio hizo za marathon ni nzuri kwa sababu mazoezi yanasaidia katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Molel amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo za hisani zilizokuwa na lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kununulia vifaa tiba wilayani Ruangwa.

Pia, Dkt. Molel ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya ambapo kwasasa asilimia 97 ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa matibabu wanatibiwa nchini.