Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda |
Na HEMEDI MUNGA
Wananchi wilayani Iramba Mkoa wa Singida, wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na mvua zilioanza kunyesha kuondokana na athari zinaweza kutokea.
Aidha, wametakiwa kuwa na tabia ya kupanda miti iwe katika mashamba au nyumba wanazojenga kwa sababu huweza kuzuwia upepo ambao unaoweza kuleta uharibufu wa mali za aina mbalimbali.
Akizungumza na baadhi ya wananchi ambao ni waumini wa dini ya kiislamu baada ya swala ya Ijumaa, Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amewataka wananchi hao kuzungushia miti katika mashamba yao.
"Ikiwa shamba lako limezungushiwa miti hata ikaja mvua yenye upepo kiasi gani mazao yako yatabaki,"amesisitiza.
Wito huo, unatokana na Watabiri wa Hali ya hewa kutabiri mvua za msimu huu zitakuwa na adha hiyo, hivyo waendelee kuchukuwa tahadhari kwa kupanda miti.
Katika hatua nyingine, Mwenda amewaomba wananchi hao kuhudhuria uzinduzi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 80 inayojengwa kwa kiwango cha lami Septemba tisa mwaka huu katika viwanja vya Misigiri.
Aidha, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa sababu ya kutenga fedha za ujenzi wa mradi ambao ni historia, haikuwahi tokea katika wilaya hiyo kuwa na barabara yenye thamani na kiwango hicho.
Amesema kuwa barabara ndio uchumi kwa sababu wenye bidhaa zao watazifikisha sokoni kwa muda sahihi na haraka huku gharama za usafirishaji zikipungua kwa sababu magari yatapita bila usumbufu.
"Ni neema kubwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutukumbuka, kwa kweli ni mradi mkubwa sana haijawahi tokea tangu kupatikana kwa uhuru, asante sana Rais wetu," ameshukuru.
Kwa upande wake Imamu wa Msikiti wa Taqwa mjini Kiomboi, Shekhe Ponda Hassan amemuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumuepushia adha na kila kisichokuwa na faida kwa wananchi Rais Dk. Samia.
Sheikh Hassan Ponda wa Msikiti wa Taqwa, Mjini Kiomboi, wilayani Iramba. |