Na Mwandishi Wetu, Rorya
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amewaeleza wanachama wa Chama hicho uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani utakuwa na ushindani hivyo wasibwete.
Akizungumza katika kikao kazi cha ndani na Wanachama wa CCM Wilaya ya Rorya mkoani Mara, ambako anaendelea na ziara ya kikazi, jana, Kinana amesema kuna kanuni za uchaguzi za vyombo vya dola.
“Tunatakiwa tufuate maadili ya uchaguzi na tufanye kila linalowezekana na nimepata ahadi nyingi kwamba tutashinda kwenye uchaguzi unaokuja wa Serikali za mitaa mwaka huu, niwambie utakuwa na ushindani.
“Kwa sababu zile sheria za uchaguzi zilizotungwa bungeni zinatoa nafasi ya ushindani, kwa hiyo tusibwete, badala yake tujipange vizuri. Tunatakiwa tujipange wanachama ili tupate ushindi wa kishindo mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema.
Kinana amesisitiza kuwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ni vema wana CCM wakashikamana na kama kuna mtu mchana yuko upande wa CCM na usiku upinzani anapaswa kuwekwa kando haraka.
“Hatuwezi kukubali watu wavae nguo za kijani mchana halafu baadaye unabadilika, hatuwezi kukubali,” amesema Kinana ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Mara.
Aidha, amesisitiza umoja na mshikamano na kama kuna changamoto zozote wanapaswa kuzizungumza kama Chama kupata ufumbuzi wake. “Tunatakiwa tushikamane na tuzingatie kanuni na katiba yetu ya CCM”, amesema.
Kuhusu viongozi ambao wamechaguliwa na sasa wako madarakani wakiwemo madiwani na wabunge, Kinana amesema waachwe wafanye kazi na hakuna sababu ya kuwavuruga.
“Kuna watu wanaitwa madalali wa vyeo, kazi yao ni kuuza vyeo anakuja kwako anakwambia mwaka ujao unatakiwa tukuchague wewe, ukisikia hivyo ujue anatafuta riziki na akimaliza kuzungumza anaomba nauli, ujue huyo ni dalali.
“Wakati mwingine anakupigia simu anakwambia hebu nirushie bando kuna habari nataka nikupe. Hao ni madali, ukija kuanguka anasema mimi nilikusaidia ila wajumbe wamekuangusha.” Ameeleza.
Amesema kwa kuwa kipindi cha uchaguzi bado hakijafika na kuna watu wanatamaa ya kuwa madiwani, ingawa jambo hilo si dhambi, lakini ni muhimu utaratibu wa Chama na kanuni mbalimbali ziheshimiwe.
AKEMEA UKABILA
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana amewasisitiza wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuachana na tabia za ukabila akieleza kuwa ni mambo ya kizamani na yanawagawa.
Akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Roria, mkoani Mara, alisema nchi kuwa na makabila ni jambo la kawaida ila ukabila ni jambo baya, akieleza kuwa kumuhukumu mtu kwa jambo ambalo hana uwezo nalo sio sahihi.
Kinana amesema hayo baada ya baadhi ya wajumbe kuibua hoja kwamba kuna mambo yanafanyika katika wilaya ya Roria ambayo yanaashiria kuwepo kwa changamoto ya ukabila miongoni mwao.
Amesema Baba wa Taifa Julius Nyerere, ametoka mkoa huo, na ni kabila dogo sana na ameongoza nchi kwa miaka 24, na kwamba alipendwa, aliheshimiwa, alithaminiwa na alitukuzwa sio kwa sababu ya ukabila bali ni kazi aliyokuwa anafanya, utendaji na uadilifu wake uliomfanya aheshimika Tanzania, Afrika na duniani.
"Sasa usimpe mtu nafasi ya uongozi kwasababu ya kabila lake, dini au umbile usimuhukumu, hayo ni mambo ya kizamani sana, tuangalie mtu anauwezo atafanya kazi atajituma na kujitolea, mnampima kwa vigezo sio kwamba huyu ni ndugu yangu.
"Mtu mmoja kwenye kabila lako akipata cheo anakusaidia nini hasa wewe mwenyewe? Uko kijijini kule mngekuwa mnagawana mshahara sawa, kila mmoja anakuletea 300,000 kutoka kwenye mshahara wake kwasababu ni kabila lako sawa... wekeni watu kwa uwezo," amesema Kinana.
Aidha, ameeleza jambo ambalo Baba wa taifa aliwaachia ni umoja wa kitaifa, akitolea mfano kwamba kuna nchi jirani, hakuzibainisha kwa majina, kwamba mtu hawezi kuwa gavana wa jimbo kama anatoka sehemu nyingine, lakini Tanzania wanafanya kazi nchi nzima.