Na HEMEDI MUNGA, Iramba
Ujio wa Madaktari Bingwa wilayani Iramba mkoani Singida, umewaibua wananchi kuendelea kumshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kutekeleza na kuboresha miradi ya afya inayotajwa kuwa msingi wa ujio wa Wataalamu hao Bobezi.
Aidha, Madaktari hao, wanatarajia kuanza kutoa huduma mbalimbali Mwezi Aprili 22, handi 25 mwaka huu katika hospitali ya Wilaya hiyo mjini hapa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao wamesema uwekezaji alioufanya Rais Dk. Samia umekua chachu cha Madaktari hao Bingwa na Bobezi kuwakumbuka wao.
Mmoja wa Wajasiriamali katika Soko la Kiomboi, Hawa Rajabu, amesema wanapokea kwa mikono miwili ujio wa wataalam hao.
"Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea jengo la wagonjwa wa dharura (emergency) na Sadaruki (ICU) ikiwemo kuleta vifaa tiba vya kisasa katika hospitali yetu," amepongeza Hawa na kuongeza kuwa:
"Itaendelea kuwasaidia wagonjwa ambao hawana uwezo wa kufuata huduma Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma au Muhimbili jijini Dar es Salaam kama ilivyokuwa zamani."
Mbali na hayo, Hawa amebainisha siku za nyuma ilikua mtu akivunjika japo mguu alitakiwa kwenda Hospitali ya Itigi au Makihungu mkoani hapa, lakini hivi sasa tiba na huduma nyinginezo mbalimbali zinapatikana katika hospitali hiyo.
"Tunamshukuru Mungu, tunamuomba aendelea kumpa afya njema Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiboresha Hospitali yetu," ameomba.
Naye, Hassan Omari amesema wananchi wa Iramba wamefurahi kwa ujio wa Madaktari hao kwa sababu watu wenye magonjwa mbalimbali licha ya kupata huduma za tiba wataepusha gharama za kufuata matibabu mbali.
Aidha, ameongeza kuwa wanamshukuru Rais Dk. Samia, Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda na viongozi wengine kwa kuwasogezea huduma za kibingwa na bobezi hospitalini kwao.
Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano wa Hadhara, Diwani wa Kata ya Old kiomboi, Sadick Mawaka amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya yenye thamani ya sh bilioni 35.576 katika kata hiyo ambayo ipo Hospitali hiyo ya wilaya inayotarajia kupokea Madaktari hao Bingwa.
Mawaka amefafanua kuwa walipokea fedha sh milioni 300 zilizojenga jengo la wagonjwa wa dharura, sh milioni 25 zilizojenga jengo la UVIKO19 na sh millioni 200 zilizomalizia Zahanati ya Kinambeu.
Ameweka wazi kuwa walipokea sh milioni 47 zilizojenga mtambo wa kuzalisha gesi ya oxygen hosptalini hapa, sh milioni 250 zilizojenga sadaruki (ICU) na sh millioni 900 za umaliziaji wa jengo la Maabara, Mama na Mtoto ikiwemo jengo la kuhifadhia Maiti.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, wamewataka wananchi wa wilaya hiyo, kuitumia fursa ya ujio wa wataalam hao.
Aidha, zimeeleza kuwa huduma zitakazo tolewa ni pamoja na Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani (TIBA, Physician), Daktari Bingwa wa Upasuaji wa jumla (General Surgeon), Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Sanifu (Plastic Surgeon), Daktari Bingwa wa Upasuaji wa mifupa (Orthopedic Surgeon) na Daktari Bingwa macho.
Pia, zimebainisha kuwa wenye magonjwa ya moyo, figo, ini, hernia, appendix, uvimbe tumboni, makovu ya majeraha ya moto, matatizo ya magonjwa ya mifupa na mengineyo watapata huduma.