Na MWANDISHI WETU
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye amefanya ziara ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dar es Salaam ikiwa ni moja ya malengo yake ya kuzitambua Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Uchukuzi, kufahamu majukumu ya kiutendaji na kuelewa changamoto zinazowakabili na mikakati ya kuimarisha taasisi na utoaji wa huduma.
Baada ya taarifa ya utendaji kutoka TMA, Naibu Katibu Mkuu, Uchukuzi aliipongeza TMA kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za haki ya hewa nchini, ikiwemo kuongeza usahihi wa utabiri, huku akieleza kuwa yeye ni mmoja wa wadau wa mamlaka hiyo kwani anafuatilia, kuzingatia na kutumia taarifa za hali ya hewa.
"Kiuekweli taarifa zenu ni nzuri, niwapongeze sana TMA, mimi ni mdau wa taarifa zenu na nimekuwa nikizifuatilia, kuzizingatia na pia kuzitumia, naweza kusema TMA ya sasa si kama ile za zamani." alisisitiza Nduhiye.
Akiwasilisha, salamu za ukaribisho Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk. Ladislaus Chang'a alieleza Maono na Mikakati ya kuimarisha huduma na kuongeza ushawishi wa TMA na Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa.
Aidha alisisitiza azma ya kuifanya Tanzania kuwa HUB ya mafunzo ya Rada za hali ya hewa katika Afrika.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Ofisi za Zanzibar, Masoud Faki alihitimisha kwa kutoa salamu za shukrani kwa kuitembelea TMA ndani ya muda mfupi tokea ateuliwe kama Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yake.