TMA yatangaza msimu wa mpya wa mvua za msimu



MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, huku ikisema kunatarajiwa mvua za wastani hadi chini ya wastani na wastani hadi juu ya wastani kunyesha maeneo mbalimbali nchini kuanzia Novemba mwaka huu hadi Aprili 2025.

Pia, imezitaka Mamlaka husika kuchukua taahadhari kulingana na taarifa hiyo ya TMA kuepusha athari zinazoweza kujitokeza kwa jamii ikiwemo vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, hususan maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

 Utabiri huo kwa vyombo vya habari, umetolewa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk. Ladislaus Chang’a.

"Baadhi ya aeneo hayo ni mikoa ya Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Kusini mwa Morogoro katika kipindi cha miezi ya Novemba, mwaka huu hadi Aprili, 2025.

"Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma, kaskazini na Mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa," amesema.

 Dk.Chang'a amesema mvua za Wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.