Itel Tanzania ya mwaga msaada Shule ya Msingi Tandale

 

Na MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Itel Tanzania imekabidhi msaada wa bidhaa mbalimbali katika Shule ya Msingi Tandale, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kurejesha pato lake  kwa wananchi.

Msaada huo ni pamoja na Kompyuta tatu, viti vya ofisi ya walimu, vitabu, madaftari, mabegi, taulo za kike, vifaa vya michezo na zawadi mbalimbali kwa wanafunzi.

Akikabidhi msaada huo, Ofisa Uhusiano wa Itel Tanzania, Sophia Msafiri, amesema ni utaratibu wa kampuni hiyo kurejesha pato lake kwa jamii hususan shule, watoto wenye mahitaji maalumu na kushiriki shughuli za kijamii.

“Itel Tanzania leo tumechagua kutoa zawadi katika Shule ya Msingi Tandale ni kawaida yetu  kusaidia shule za msingi na sekondari. Pia tunasaidia  vituo vya yatima na shughuli za kijamii", amesema Sophia.

Sophia amesema kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono jamii kupitia utaratibu huo wa kurejesha faida inayopata.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tandale, Andrew John, ameishukuru Itel Tanzania kwa msaada huo na kueleza utasaidia utoaji wa elimu.

Amesema shule hiyo inazaidi ya wanafunzi 2000 na inaongoza kwa kufaulisha wanafunzi  wilayani Kinondoni, hivyo msaada huo utaongeza ufanisi.