Na Mwandishi wetu, Kongwa, Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewasihi wazazi kuwahamasisha na kuwasimamia watoto kusoma vizuri ili waweze kusimamia maendeleo ya uchumi yanayotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Masauni ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2024 wakati akizindua Jengo la Maabara katika shule ya Sekondari Laikala, Wilaya ya Kongwa, Dodoma ambapo amesema "Uchumi wa Nchi yetu unatanuka sana na hivyo tunahitaji ushiriki na mchango mkubwa wa wananchi hivyo nivema vijana wakaandaliwa vizuri waweze kushiriki".
Wakati huo huo Mhandisi Masauni amesisitiza wanafunzi kutumia fursa hiyo ya shule na Maabara ya kisasa kusoma masomo ya sayansi.
Makadirio ya Ujenzi wa Maabara hiyo yalikuwa ni Tsh Milioni 60 lakini Ujenzi wake mpaka kukamilika umegharimu Tsh Milioni 57.8 na fedha iliyobaki ni Tsh Milioni 2.2, maabara hiyo inaweza kutumika kwa masomo ya baiolojia, fizikia na kemia kwa nyakati tofauti tofauti.