MTU
MISHI wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Eben-Ezery Mende, amejitokeza kugombea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Akizungumza na jijini Dar es Salaam, Mende amesema amewiwa kuigombea nafasi hiyo kwa kuwa uongozi ni karama aliyotunukiwa na Mungu na anaamini ataitendea haki nafasi hiyo.
"Si kila mtu ana karama ya uongozi na waliopewa karama hiyo wasipoitendea kazi watadaiwa siku ya mwisho. Mungu alienipa tunu hiyo ndiye atakaehusika ndani yangu" amesema Mende.
Alisema watumishi nchini wamepungua msisimko wa kufanyakazi kwa sababu nyingi ikiwemo ya watu wanaopaswa kuamsha msisimuo huo kutulia.
Pia amesema akipata nafasi hiyo atahakikisha utaratibu wa wajibu na haki vinazingatiwa kama ilivyo utaratibu wa tamakali ya nahau hiyo.
Amewaahidi watumishi wote nchini kukaa mkao wa furaha na matumaini kwa kuwa tumaini la matarajio yao limewafikia.
Uchaguzi huo utafanyika jijini Dodoma Novemba 14 mwaka huu kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Cornel Maghembe aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa Mende, TUCTA ni taasisi kubwa inayohitaji umakini mkubwa kiuongozi na kwa namna alivyojipima amejiridhisha kwamba ataiongoza vema na kuweka historia nzuri ya kiuongozi.
Mende ambaye kitaaluma ni Mwandishi wa Habari amewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO) Mkoa wa Shinyanga.