Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewapongeza wafanyabiashara 19 kutoka Tanzania ambao walishiriki maonesho ya kibiashara kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu la Afrika na Urusi lililomalizika Julai 28, mwaka huu.
Wafanyabiashara hao wanamiliki makampuni yanayohusika na sekta za elimu, afya, kilimo, madini, mafuta na gesi, utalii, ujenzi, utafiti na ushauri wa kibiashara.
Ametoa pongezi hizo jana jioni (Jumamosi, Julai 29, 2023) wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.
“Nawapongeza kwa kuamua kusafiri na kuja hadi huku ili kutumia fursa ya mkutano wa Urusi na Afrika kutafuta masoko ya bidhaa zenu na wabia wa kufanya nao biashara kule nyumbani. Sekta binafsi ya pande zote mbili za nchi yetu ni muhimu. Nataka mtambue kuwa mna mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa letu,” amesema.
“Udhahiri wa sekta binafsi umeonekana leo kwa kitendo chenu cha kushiriki Expo Forum na mimi nataka niwathibitishie kuwa mnao uwezo mkubwa wa kutafuta mitaji na rasilmali mbalimbali. Niwasihi muungane mkono ili muweze kuwafikia wazalishaji wakubwa huku mkiwaeleza kuwa Tanzania ni nchi iliyokaa kimkakati kwenye sekta ya kibiashara,” amesema.
Amewaambia wafanyabiashara hao kwamba Serikali inathamini majukumu yao na kwamba itawaunga mkono ili waweze kuendelea kufanya vizuri. “Anzisheni viwanda, boresheni biashara zenu na mkutane na wawekezaji mbalimbali,” amesisitiza.
Pia amewapa nafasi wafanyabiashara hao watoe maoni yao kuhusiana na ushiriki wao kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu ili Serikali iweze kuyafanyia kazi.
Akisoma risala kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Bw. Otieno Igogo alisema walikuja na bidhaa mbalimbali ili kuzitangaza na kutafuta fursa za kibiashara kwenye soko la Urusi.
Amezitaja bidhaa hizo kuwa ni korosho, mafuta ya alizeti, kahawa, rosella, viungo mbalimbali (spices), mchele, karanga, vanilla, madini mbalimbali, zabibu na mvinyo. “Kati ya hizo, kuna bidhaa ambazo zimependwa zaidi ikiwemo korosho, kahawa, viungo (spices), rosella, karanga, mchele, mafuta ya alizeti na zabibu.”
Igogo alimweleza Waziri Mkuu kwamba makampuni 10 kati ya 19 yaliyoshirki kongamano hilo kutoka Tanzania, yameweza kusaini mikataba ya ushirikiano wa kibishara na makampuni 11 toka Urusi ilhali makampuni mengine matano bado yako kwenye maongezi ya ushirika wa kibiashara.
“Baadhi ya makampuni yaliyoshiriki kongamano hili yamefanikiwa kufanya makubaliano ya ushirikiano na mengine yako kwenye maongezi ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukaushaji wa matunda, uchimbaji na utafiti wa madini, mafuta na gesi, uanzishaji wa viwanda kwa ubia kwenye maeneo ya uchakataji na utengenezaji wa engineered wood product na mitambo kwa ajili ya kilimo cha kisasa.
Pia kuna baadhi ya kampuni ambazo zimesaini mikataba ya uwezeshaji katika masuala ya uwekezaji baina ya wafanya biashara wa Urusi na Tanzania.” Alisema.
Mkutano huo uilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.