Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya madini ya Barrick Bulyanhulu, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, imeviwezesha vikundi 11 vya wajasiriamali wa kilimo na ufugaji kushiriki katika Maonyesho ya Kilimo Kanda ya ziwa Mashariki, mkoani Simiyu.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana, katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi, Ofisa Uhusiano wa Jamii wa kampuni hiyo, Mary Lupamba, amesema vikundi vilivyowezeshwa ni kutoka maeneo ya jirani ya mgodi huo, ili wapate masoko ya bidhaa zao.
Mary amesema mgodi huo umeamua kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta ya kilimo na ufugaji kwa kuwawezesha kupata masoko, hiyo inatokana na wakulima na wafugaji huzalisha bidhaa mbalimbali lakini hukabiliwa na changamoto ya kukosa soko la bidhaa zao.
"Sisi mgodi kwa kushirikiana na halmashauri ya Msalala tumeonelea kwamba maonyesho haya ya nanenane ni fursa na eneo ambalo lina wananchi wengi na wadau wengi wa kilimo na ufugaji tukaona ni vizuri tuweze kuja nao wao wenyewe, wajifunze masuala mengine ya kilimo na mifugo na kutengeneza mitandao ya masoko ya bidhaa zao", amesema.
Pia Mary amesema mgodi wa Barrick Bulyanhulu umesajili zaidi ya wajasiriamali 40 kutoka vijijini jirani na mgodi katika mfumo wa zabuni wa mgodi kuuza bidhaa zao mgodini na wamekuwa wakiwawezesha kuwapa mafunzo ya ujasiriamali mbalimbali wanaofikia zaidi ya 500.
Amesema vikundi hivyo vilivyowezeshwa katika maonyesho hayo wamenufaika na fursa mbalimbali zikiwemo kukagua mashamba ya mfano, kuzalisha kwa tija na ufugaji wa kisasa.
Mmoja wa wajasiriamali kutoka katika vikundi vilivyowezeshwa, Hussein Malimi, amesema maonyesho hayo yamewaongezea kupata mtandao wa masoko na kujifunza mambo mbalimbali mapya.
"Ujio wangu hapa katika maonyesho haya nimefanikiwa kukutana na watumiaji wapya wa bidhaa zangu za asali na wenzagu wameweza kuuza bidhaa zao mbalimbali na kupata oda mpya”,alisema Hussein.
Kwa upande wake mfugaji nyuki, Samuel Igoko, amesema fursa ya kushiriki maonyesho hayo imempa nafasi ya kujitangaza na kupanua zaidi soko la bidhaa zake.
“Tunashukuru kampuni ya Barrick kwa kutuwezesha kufika hapa na kushiriki maonesho haya, yametuwezesha kukutana na watu wengi na kujitangaza na hii inadhihirisha kuwa uwekezaji wa Barrick katika eneo letu unazidi kutunufaisha wananchi”, amesema.