Wananchi wakimbeba kwa furaha Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman, Mwenda, baada ya kuzindua Zahanati katika Kijiji cha Ndurumo, Kata ya Kidaru mkoani Singida. (Picha na Hemedi Munga). |
Na HEMEDI MUNGA
Juhudi za wananchi wa Kijiji cha Ndurumo Kata ya Kidaru wilayani Iramba mkoani Singida zimewaibua viongozi kumalisha ujenzi wa zahanati kwa lengo la kufikisha huduma za afya karibu na wananchi.
Halmashauri ya wilaya hiyo imetoa takribani sh milioni 79 ambazo zimekamilisha ujenzi wa Zahanati ambayo ameizindua Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda.
Akizungumza katika hafla hiyo baada ya uzinduzi wa Zahanati hiyo katika kijiji hicho, Mwenda ameupongeza uongozi wao na Mwenytekiti wa Halmashauri hiyo, Innocent Msengi kwa kukamilisha Zahanati 10 na usimamiaji madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Pia, amempongeza Mbunge wa jimbo hilo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba kwa kuhakikisha anawasemea watu wake bungeni na kufanikisha kupata fedha za kujenga vituo vya afya sita ndani ya miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
"Ndugu zangu hakika Rais Dk. Samia ametekeleza wajibu wake kwa kuboresha huduma za afya," amesema.
Aidha, amesema kwa upande wa sekta ya nishati ya umeme Rais Dk. Samia amehakikisha umeme unafika katika kila kijiji huku akiahidi kufikisha katika kila kitongoji.
" Baada ya miezi miwili umeme utafika hapa na katika kila kitongoji kati ya vitongoji 393 vya wilaya hiyo vyote vitapata umeme," amesema Mwenda.
Amesema Rais Dk. Samia ameleta takribani sh milioni 800 kwa lengo la kununua vifaa tiba na leo mmeona vifaa pea tatu tatu zipo katika zahanati hii.
Pia, barabara mpango wa serikali ni kujenga barabara ya kutoka Shelui hadi Sibiti na barabara ya kutoka Kizaga hadi Singida mjini kwa kiwango cha lami.
" Huyo ndio Rais Dk. Samia anayafanya makubwa kwa wananchi wake," amesisitiza.
Mwenda ameomba namna pekee ya kumlipa rais huyo ni kumpa kura za kishindo kwa lengo la kuendelea kupata huduma hizo karibu na kwa wakati.
Pia, amewaasa wananchi hao na viongozi wa Kimila kuwapa ulinzi wa siri na dhahiri huku akionya kutosikia watumishi hao wanalala ndani wanajikuta wako nje.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Msengi amesema hitajio la jamii liliwasukuma wao kutoa fedha kukamilisha ujenzi huo.
" Bila kusita kwa sababu nilifia mwenyewe na kuona nguvu ya jamii, umuhimu wa jambo hili nilishawishi kupata sh milioni 79 za ujenzi huu," amesema.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Philipo Manguli amemuomba Mkuu wa Wilaya kuwafikishia salamu kwa Rais Dk. Samia kwa kuwapa fedha za kukamilisha bweni zaidi ya sh milioni 80, fedha za kujenga madarasa zaidi ya sh milioni 100, kujenga jengo la kujifungulia sh milioni 90, sh milioni 250 kujenga nyumba za walimu na matundu ya vyoo katika kijiji cha Mwamapuli.
"Hizi ni fedha za Dk. Samia na tutamuonesha upendo wetu kwenye sanduku la kupiga kura, 2025," amesema.
Ameongeza kuwa Dk. Samia amejiatahidi kufungua uchumi na kufanikisha wao kupata fedha nyingi zinazosaidia kutatua kero za wananchi kwa wakati.
"Tunamuhakikishia rais wetu 2025 kura zote zakwake aendelea kututumikia tupate maendeleo," amesisitiza.
Naye Mzee wa Jadi, Chandika Halawa, Amewaomba wananchi kuheshimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kwa sababu ni mfano wa baba na mama kuwajali wananchi wake.
Amesema haijawi kutokea tangu mwaka 1973 alipozaliwa kijiji hicho kupata huduma hiyo.
Zahanati ya Kijiji cha Ndurumo Kata ya Kidaru wilayani Iramba mkoani Singida, iliyozinduliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mwenda. |