Na MWANDISHI WETU
WADAU wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wameiomba Serikali kupatia suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani barabara ya Serengeti
Akizungumza leo na waandishi wa habari ambao wametembelea eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TANAPA katika kuboresha barabara hizo, ambazo ziliathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua na wingi wa magari ya utalii yanayopita kwa siku takribani magari 300 hadi 500 yaliyobeba watalii yanatumia barabara hiyo.
Macha aliyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika barabara ya Naabi hadi Seronera.
“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zilizonyesha tofauti na miaka mingine.