Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wakulima kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha na kuuza ziada kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili wapate faida.
Rais Samia amesema hayo wakati wa kilele cha Maonyesho ya Kilimo na maadhimisho ya sherehe za Nanenane, yaliofanyika katika viwanja vya John Mwakangale.
Amesema serikali imedhamiria kuwa na uwezo wa kuhifadhi chakula tani milioni 3, ifikapo mwaka 2030 ili kusaidia nyakati za dharura.
Aidha Rais Samia amesema inaendelea kufanya jitihada za makusudi za kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo kwa kuwa kundi hilo ndiyo nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Pia Rais Samia amesema jitihada hizo ni pamoja na kuanzishwa programu ya miaka minane inayoitwa 'Building a Better Tommorrow' (BBT), ambapo vijana 812 kati yao wanawake 282 na wanaume 520 wanaendelea na awamu ya kwanza ya mafunzo ya kilimo biashara katika vituo atamizi 13.
Vile vile Rais Samia amesema juhudi hizi zimeifanya Tanzania kutambulika kimataifa na kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Jukwa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (Africa Food System Forum) litakalofanyika Septemba 5 had 8 mwaka jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amesema jukwaa hilo litaipatia Tanzania fursa za kibiashara na kuongeza ushirikiano nchi za Afrika kwakuwa na mifumo jumuishi ya kuimarisha kilimo, mifugo na uvuvi itakayochochea zaidi, ajira, uwekezaji na ukuaji kiuchumi.