MFANYABIASHARA GEITA AELEZA ELIMU YA KODI ILIVYOMSAIDIA KUOKOA WENZAKE KUTAPELIWA NA VISHOKA

NA MWANDSHI WETU

Mfanyabiashara wa mkoani Geita, Marik Ngutti,  ametoa ushahidi wa namna alivyotumia elimu ya kodi  kuwaokoa wafanyabiashara wenzake wa machimbo ya Matabi, Wilaya ya Chato, mkoani Geita,  kwa kuwabaini Vishoka, wanaojitambulisha Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ngutti alitoa ushahidi huo alipotembelea katika banda ya la TRA kuongeza elimu ya kodi, wakati wa Maonyesho ya Wakandarasi yanayoendelea katika viwanja vya EPZ Bombambili, mkoani humo.

Amesema walikuja watu waliojitambulisha kuwa wao ni maofisa na kuomba fedha kutoka wafanyabiashara wenzake kwa lengo la kuomba fedha kutoka kwa wafanyabiashara.

Ngutti amesema baada kuwakuta watu aliwatilia shaka na kuanza kuwahoji maswali ikiwemo kuwaomba vitambulisho vyao vya kazi.

Alisema watu hao 'vishoka' walitaka wapewe malipo mkononi na badala yake siyo katika mfumo wa mtandao kwa kutumia namba maalumu ya malipo, ndipo alipowagundua siyo maofisa wa TRA.

"Wenzangu walikuwa tayari kutoa fedha ila mimi niliwatiliashaka na kuanza kuwaomba vitambulisho vyao, nikagundua hawa siyo maofisa wa TRA na nikapiga simu TRA kuthibitisha kama nikweli maofisa wao, watu wakaondoka eneo hilo", amesema.

Aidha Ngutti amewashauri wafanyabiashara na wananchi wawe na utaratibu wa kutembelea katika banda la maonesho la mamlaka hiyo katika maonyesho mbalimbali, kushiriki semina za elimu ya kodi na kufuatilia vipindi vya elimu ya kodi kutoka TRA, ili wapate elimu ya kodi.