Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Orxy Energies, Benoit Araman. |
NA MWANDISHI WETU
Kampuni ya Oryx Energies Tanzania, imeunga mkono juhudi za serikali katika matumzi ya nishati safi kwa kugawa mitungi ya gesi ya kilo 15 na majiko ya sahani mbili kwa wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mitungi hiyo, Kigamboni, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Benoit Araman, amesema lengo la kugawa mitungi na majiko ni muendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha matumizi ya gesi yanaongezeka nchini.
Araman amesema kampuni hiyo imekuwa inafanya kampeni maalumu mbalimbali ya kuhamasisha jamii kutumia nishati safi, kwa kugawa mitungi ya gesi bure katika jamii.
"Waandishi wa habari mna mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya, wanafanya kazi kubwa ya kuuhabarisha umma, kwa kutambua mchango wao Oryx tumeona ni busara kugawa mitungi kwa wadau hawa muhimu", amesema.
Amesema dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kuona ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, hivyo Kampuni ya Oryx imedhamiria kwa vitendo kufanikisha ndoto hiyo.
Pia Araman amesema wataendelea na kampeni hiyo kadri ya uwezo wao ikiwa lengo ni kufikiwa wananchi wengi zaidi nchini nzima, wameshagawa mitungi ya gesi zaidi ya 33,000 maeneo mbalimbali, ambapo Sh. bilioni 1.5 kimeshatumika.
Amesema wanakabidhi mitungi hiyo kwa wahariri na waandishi kwasababu wana ushawishi na watasaidia kuhamasisha jamii katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.