RAIS DK. SAMIA: SERIKALI INAJUKUMU LA KUWASHIRIKISHA WATANZANIA HISTORIA NA KUMBUKIZI YA VIONGOZI WALIOTANGULIA MBELE ZA HAKI

 


Na HEMEDI MUNGA

RAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali inayojukumu la kuwashirikisha watanzania  historia na kumbukizi za viongozi waliotangulia mbele ya haki.

Dk. Samia ametoa kauli hiyo, wakati akishiriki Misa Maalumu ya Kumbukizi ya Miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine, iliyofanyika kwenye makazi ya familia yake Monduli, mkoani Arusha.

Amesema Hayati Sokoine alikuwa kielelezo cha kiongozi mzalendo, mchapakazi, mwajibikaji na mwadilifu kwa umma wa Watanzania.

"Tunafanya kumbukizi hizi katika historia ya nchi yetu kwani zinachangia mizizi ya uimara wetu," amesisitiza Dk. Samia.

Aidha, ameeleza kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zinaonesha asilimia 81 ya Watanzania walizaliwa baada ya kifo cha Mhe. Sokoine, hivyo Serikali inalo jukumu la kuwashirikisha historia na kumbukizi hizi. 

Pia, ameongeza kuwa kumbukizi hizi zinawakumbusha wapi wametoka, wapi walipo, wapi wanataka kufika na nini wafanye kwa lengo la kuhakikisha wanafika, kwa mujibu wa mafunzo ya njia ya waliowatangulia. 

Katika hatua nyingine, Dk. Samia ameiagiza  Wizara ya Utumishi kuendelea kutunza kumbukumbu za viongozi wao hawa na kuhakikisha historia, rekodi na mafunzo ya umahiri wa utumishi wao unaifikia jamii.

"Nimeagiza Wizara ya Utumishi kuendelea kutunza kumbukumbu za viongozi wetu hawa na kuhakikisha historia, rekodi na mafunzo ya umahiri wa utumishi wao unafikia jamii, hasa vijana," amesema.

Hatua hiyo itawapa mwanga wa kujifunza wametoka wapi na wapi wanapaswa kwenda kama Taifa katika utumishi wa umma na jamii kwa ujumla.