RC CHALAMILA AKERWA NA MKANDARASI KUCHELEWESHA MRADI BRT-3

NA MWANDISHI WETU

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema haridhishwi na kasi ya mkandarasi  kampuni ya Sinohydro ya China inayojenga miundombinu ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu yatatu ( BRT-3) na kutishia  kuwaweka mahabusu.

Aidha ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)  kusimamia kikamilifu mradi huo  hususan mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana.

Chalamila amesema hayo jana, alipokagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa katika Barabara ya Nyerere na kuishia Gongo la mboto.

Amesema hafurahishwi na kasi ya utendaji ya mkandarasi na hakubaliani na utetezi wa mkandarasi  huyo kukwamishwa na mvua inayoendelea kunyesha.

“Nitawaweka ndani wakandarasi. Sifurahishwi na kasi ya ujenzi wa  huu mradi. Hicho ndiyo kimenileta.Sifurahishwi na kasi ya mkandarasi.”amesema Chalamila.

Ameeleza, mvua haiwezi kuwa kikwazo cha mkandarasi  kutekeleza mradi huo kwa wakati kwani  anaweza kufidia muda kwa kufanya kazi zake kuanzia asubuhi mpaka usiku.

“Mmesema mkandarasi anafanya kazi zake mpaka usiku siyo kweili. Hafanyi kazi usiku.  Tumefanya ziara za kushitukiza na Mkuu wa Wilaya ya Ilala hapa (Edward Mpogolo), hatujawahi kumkuta mkandarasi anafanya kazi usiku,”alieleza Chalamila.

Amesema, kitendo cha mradi huo wa BRT-3 kuto kutekelezwa kwa wakati kunasababisha changamoto kubwa ya usafiri kwa wananchi  hasa wa Gongo la mboto na maeneo jirani.

“Wananchi wanahangaika usafiri. Waanahangaika na treni. Wanataka mradi huu umalizike. Msimamieni  ningeweza kuwaweka ndani hata nyie TANROADS.Kama changamoto ni mvua kwa nini asifanye kazi mapema asubuhi mpaka usiku,”alisema mkuu huyo wa mkoa.

Amesisitiza mkandarasi kumaliza  mradi kwa wakati kwani miezi 12 aliyoongezwa inatosha  kukamilisha mradi huo muhimu.

Katika hatua nyingine Chalamila aliitaka TANROADS kuanisha  hifadhi zake za barabara kwa kuziwekea alama  kwani Mkoa wa Dar es Salaam, una malengo ya kupanda miti na kujenga bustani kando ya barabara zake kuboresha mazingira na mandhari.

“Nataka kila eneo lililombele katika barabara lipandwe miti.  Tuwe na sehemu nzuri za kupumzikia na kunywa kahawa. Tunataka kutekeleza mkakati huo na ninaelekeza watendaji na viongozi wa kata ambao maeneo yao yako barabarani  kuwa na mkakati huo wa uboreshaji wa maeneo hayo,”alisema.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema mradi huo ukikamilika utaleta tija kubwa kwa wananchi na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Meneja wa TANROADS  Mhandisi Frank Mbilinyi, amesema ujenzi wa mradi huo wa BRT-3 umefikia asilimia 45.3.

Mhandisi Mbilinyi, amesema   ujenzi unahusisha Kilomita 23.3 na gharama yake ni sh. bilioni 231.6 na kwamba mradi ulikuwa  miezi 20 tangu mwaka 2022 mkataba uliposainiwa.

“MKandarasi ameongezewa muda wa miezi 12 hivyo mradi  utakamilika mwakani,”alisema  Mhandisi Mbilinyi.

Alisema kasi ya mhandisi kutekeleza mradi huo ni kubwa na amekuwa akifanya kazi usiku na mchana, ikiwemo kuongeza nguvu kazi na mitambo.