Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego |
Watumishi mkoani Singida, wametakiwa kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kufanya kazi kwa weledi na bidii huku madeni yao yakiendelea kulipwa.
Mkuu wa mkoa huo, Halima Dendego, ametoa wito huo katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi 'Mei Mosi', wilayani Ikungi, mkoani humo, Uwanja wa Stendi ya zamani.
Amesema wakati anakabidhiwa Singida, Sh. milioni 700 zimetumika kulipa madeni limbikizi kwa watumishi wa mkoa huo.
Halima amemshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya dhati kushughulikia madeni mbalimbali yakiwemo ya watumishi.
Amesema dhamira ya serikali ni kuendelea kusimamia na kuhakiki stahiki kwa lengo la kuwalipa watumishi wote wanaodai madeni yao.
"Ndugu zangu Wafanyakazi, tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumeona upandaji wa madaraja kwa mserereko, punguzo la kodi kwa asilimia moja na kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi", amesema.
Aidha, amewataka waendelee kuunga mkono juhudi za serikali kwa sababu wanaona dhamira njema ya kumfanya mfanyakazi wa Singida na Tanzania kwa ujumla kufanya kazi katika mazingira rafiki.
Halima amewaagiza waajiri wote mkoani humo kuhakikisha wanaitisha Mabaraza ya wafanyakazi mara moja kwa sababu yapo kisheria.
"Ninawaagiza wote wanaotakiwa kufanya hivyo, wafanye mara moja, mimi siyo muumini wa watu wanaopenda kuvunja sheria, ambao hawafanyi mabaraza mwisho ni siku hii ya leo, hujafanya mimi nitaanza na wewe", amesema.
Amesema watu wanaowaongoza wanayo mawazo mazuri, hivyo watoe fursa ya kuwasikiliza kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi.
Kwa upande wa Katibu wa CCM mkoani humo, Lucy Shee, amesema wanajivunia kwa sababu wafanyakazi hao wanatekeleza Ilani ya Chama.
Amesema mkoani humo Ilani ya CCM imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, na kuwapongeza watumishi kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya.
Lucy amesema Rais Dk. Samia, ameleta miradi mingi ambayo imetekelezwa na kuwafanya watembee kifua mbele na kuwataka waendelee kumuunga mkono Rais Dk. Samia, kwa kufanya kazi kwa bidii.
"Tuendelee kumuheshimisha, tumsemee, tumlinde na tusikubali watu wabaya wenye nia mbaya na nchi yetu wakamuhujumu Rais wetu", amesema.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Shee |